• Welcome

  • ULEGA ATOA SIKU 30 KWA MKANDARASI BARABARA YA NSALAGA - IFISI KUWEKWA LAMI

    ULEGA ATOA SIKU 30 KWA MKANDARASI BARABARA YA NSALAGA - IFISI KUWEKWA LAMI Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa siku 30 na kumtaka Mkandarasi Kampuni ya CHICO anayetekeleza ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Nsalaga - Ifisi (km 29) kwa njia nne, jijini Mbeya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo. Aidha, Waziri Ulega amemuagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza vifaa pamoja wafanyakazi ili kufanikisha mradi huo ukamilike haraka iwezekanavyo. Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Mbeya wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na hatua za utekelezaji wake ambao hadi sasa umefikia asilimia 25. Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imeshatoa malipo ya Shilingi Bilioni 35 kwa Mkandarasi huyo na matarajio yake ni kuona kupitia fedha hizo angalau kilometa kadhaa za lami zimekamilishwa kujengwa katika barabara hiyo. “Serikali imeshatoa Bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Nsalaga hadi Ifisi, na fedha hizi Mkandarasi hajazifanyia kazi ipasavyo, Sasa basi Nimemuagiza Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuona mabadiliko ya haraka katika mradi huu”, amesisitiza Ulega. Pia, ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu ili hadi kufikia mwanzoni mwa Mwezi Juni mwaka huu Mkandarasi awe amekamilisha kilometa 10 za lami katika barabara hiyo na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kukagua maendeleo hayo. Ulega amemuelekeza Meneja huyo wa TANROADS kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaenda sambamba na ufungaji wa taa za barabarani ili kuupendezesha mji wa Mbeya na kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama wa wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku. Vilevile, Ulega amepokea Ombi la Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson la ujenzi wa kilometa tano za lami zinazoingia katika mitaa ya iiji la Mbeya na kuahidi kulifanyia kazi. Kadhalika, Ulega amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi katika kuhakikisha kazi ndogondogo zinazofanywa na Mkandarasi zinatolewa kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya ili kutoa fursa za ajira na vijana hao waweze kunufaika na matunda ya mradi. kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameeleza kuwa wananchi wa Mbeya wamekuwa wakisubiri kwa hamu upanuzi wa barabara hiyo kukamilika ili kutatua changamoto za msongamano wa magari jijini humo. Dkt. Tulia ameiomba Wizara ya Ujenzi kufanyia kazi mapendekezo yaliyoombwa katika barabara hiyo ya kuongezwa kwa barabara kilometa 3.5 kuanzia Ifisi hadi Songwe Airport na kilometa 5 kuanzia Nsalaga kuelekea Mlima Nyoka katika Bajeti mpya ya mwaka 2025/26 ili wananchi wa Mbeya kuendelea kunufaika na ujenzi wa mtandao wa barabara jijini humo. Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige ameeleza kuwa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa matabaka ya udongo G3, G7 na G15, ujenzi wa makalvati madogo na makubwa pamoja na ujenzi wa daraja la Nzovwe katika barabara hiyo.

  • BASHUNGWA AIAGIZA TANROADS KUFUNGA MIZANI MITATU YA KUPIMA UZITO WA MAGARI TUNDUMA

    BASHUNGWA AIAGIZA TANROADS KUFUNGA MIZANI MITATU YA KUPIMA UZITO WA MAGARI TUNDUMA

  • KASEKENYA ATOA MIEZI MIWILI UJENZI OSBP KASUMULU UKAMILIKE

    KASEKENYA ATOA MIEZI MIWILI UJENZI OSBP KASUMULU UKAMILIKE

  • Makamu wa Rais akagua barabara mchepuko ya Inyala

    Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amekagua barabara ya mchepuo wa Inyala yenye kilometa 2.8 na Upanuzi wa Barabara ya TANZAM sehemu ya Inyala - Shamwengo yenye kilometa 3 jijini Mbeya.

  • UJENZI WA BARABARA YA NJIA NNE MBEYA WAANZA

    Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ametaka usimamizi madhubuti wa Ujenzi wa Barabara ya Igawa - Songwe – Tunduma, Sehemu ya
    3, Ujenzi wa Njia Nne kutoka Nsalaga (Uyole) mpaka Ifisi (Kiwanja cha Ndege cha Songwe) yenye urefu wa kilometa 29.

  • KM 32 WILAYANI KYELA KUJENGWA KWA LAMI

    Serikali imesema itaendelea kutekeleza Sera yake ya kuunganisha mkoa kwa mkoa na wilaya kwa wilaya kwa barabara za lami ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria, mazao na malighafi mbalimbali ili kukuza uchumi kwa haraka.