• Welcome

  • DARAJA JIPYA LA WAMI LAANZA KUTUMIKA

    Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameruhusu Magari kuanza kutumia daraja jipya la Wami kufuatia ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 96. Waziri Mbarawa amewetaka madereva na watumiaji wa daraja walitunze ili liweze kudumu miaka 120 kama lilivyo sanifiwa. “Sisi kama Wizara, TANROADS pamoja na wananchi wa maeneo haya tuna kazi kubwa ya kulinda Daraja hili, ili tuwatende haki Watanzania wenzetu na vizazi vya baadae”. Alisema Prof Mbarawa. Aidha Prof. Mbarawa aliongeza kwa kusema “Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi inasimamia miradi mbalimbali ya kimkakati nchi nzima kwa lengo la kuifungua nchi kiuchumi na kwa miradi ya Pwani ifikapo mwaka 2025 barabara ya Bagamoyo – Pangani – Tanga – Horohoro hadi Lungalunga (Kenya) itakuwa imekamilika”. ” Serikali pia itajenga barabara za kisasa ya magari yaendayo haraka kuanzia Kibaha – Chalinze – Morogoro Express Way yenye urefu wa kilometa 215” alisema Prof. Mbarawa. Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Dorothy Mtenga, amesema zaidi ya shillngi billioni 75 zimetumika katika ujenzi wa Daraja Jipya la Wami. Aidha daraja la zamani lilikuwa halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka 63 iliyopita na lilikuwa na njia moja. Naye Mkuu wa Wilaya wa Bagamoyo, Bi Zainabu Abdallah Issa, ameishukuru Serikali hususan Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa utekelezaji wa miradi ya miundombinu. Amemhakikisha Waziri Mbarawa kuwa madaraja na barabara zinazojengwa katika mkoa wa Pwani zinatunzwa vizuri. Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameishukuru Serikali kwa kuendeleza miradi ya miundombinu katika mkoa wa Pwani ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo. Daraja jipya la Wami, lenye urefu wa mita 513.5, upana mita 11.85 na barabara unganishi km 3.8 linaunganisha mkoa wa Pwani na Tanga. Kukamilika kwake kutachochea fursa zaidi za kiuchumi na kuleta maendeleo kwa mikoa ya kaskazini mwa Tanzania