News

TANROADS MKOA WA DODOMA YAFUNGA TAA ZA KISASA ZA KUVUKA BARABARA KWA WATEMBEA KWA MIGUU (PUSH BUTTON PEDESTRIAN CROSSING)

TANROADS MKOA WA DODOMA YAFUNGA TAA ZA KISASA ZA KUVUKA BARABARA KWA WATEMBEA KWA MIGUU (PUSH BUTTON PEDESTRIAN CROSSING)

Dodoma, 14 Machi, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dodoma imefunga taa za kisasa maalum kwa kivuko cha watembea kwa miguu (Push button pedestrian crossing), ambao watavuka kutoka upande mmoja wa barabara na kwenda upande mwingine.

Mhandisi Christina Nyamziga, ambaye ni Msimamizi wa Kitengo cha Mipango ambaye anashughulikia maswala ya usalama barabarani kutoka TANROADS Dodoma, amesema taa hizo za kisasa zenye kuruhusu mvukaji wa barabara kusimamisha vyombo vya moto na kuvuka salama zimefungwa kwenye barabara kuu ya Dodoma - Bereko na Gairo - Dodoma.

Amesema taa hizo zimefungwa kwenye maeneo ya Chuo cha Mipango na Ihumwa penye shule ya msingi Jenerali Musuguri, ambapo awali wanafunzi walikuwa wakipata ajali kwa kugongwa na magari na pikipiki na kusababishiwa majeraha, ulemavu na hata kifo.

“Hizi taa ni za kisasa kabisa na zimefungwa kwanza katika maeneo hayo ambayo yanatumiwa na watu wengi wakiwemo wanafunzi wa Chuo cha Mipango na shule ya msingi Jenerali Musuguri, ambapo wamekuwa wahanga wakubwa wa kugongwa na magari, bajaj na bodaboda mara kwa mara na kuwasababishia ulemavu wa kudumu na wakati mwingine vifo,” amesema Mhandisi Christina.

Amesema tayari wanafunzi wa chuo na shule hiyo ya msingi wamepata mafunzo kutoka kwa wataalam namna bora ya kutumia kitufe maalum kinachozuia magari kwa kuwaka taa nyekundu zilizopo juu kwenye mlingoti na alama ya mtu mwenye rangi ya kijani akitembea katika mduara ulipo katikati ya mlingoni kwa kulia na kushoto zikiwaruhusu watumiaji kuvuka barabara kwa usalama zaidi.

Hatahivyo, ametoa wito kwa watumiaji wa maeneo hayo kuwa makini na matumizi ya kubonyeza kitufe na wasiharibu miundombinu hiyo, ambayo ni muhimu kwa kusaidia watembea kwa miguu wote.

Kwa upande wake Kaimu Msimamizi wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Dodoma, Mhandisi Filbert Biseko, amesema taa hizo zitakuwa mkombozi kwa wanafunzi wa Chuo cha Mipango na shule ya msingi kwa kuwa watawahi madarasani, maana awali walitumia muda mrefu kuvuka barabara, ambazo zinatumiwa na magari mengi yakiwemo malori makubwa ya mizigo, mabasi ya abiria, magari madogo binafsi na ya serikali, bajaj na bodaboda.

“Mahali hapa zilipofungwa taa palikuwa ni sehemu hatarishi kwa maisha ya wanafunzi hawa na watu wengine, pamoja na kwamba awali kulikuwa na alama ya pundamilia inayowaruhusu kuvuka baada ya magari kusimama kama vibao vinavyoelekeza, lakini bado kuna madereva wengine walikuwa wakikiuka taratibu na masharti wakifika eneo hilo, na kuendelea na safari zao bila kuwajali wanaovuka, na hao ndio wanasababisha ajali za kuwagonga,” amesema Mhandisi Filbert.

 Amesema pia katika maeneo hayo kumekuwa na ajali za mara kwa mara kwa magari yenyewe kwa wenyewe kugongana wakiwa kwenye mwendokasi bila kuzingatia alama za barabarani.

 Halikadhalika, Mhandisi Filbert amesema taa kama hizo pia zitafungwa kwenye maeneo ya Vikonje na Mnada Mpya, ambapo napo watumiaji wa barabara hiyo wanaathirika kwa kugongwa na vyombo vya moto.

Naye Mhandisi Leonard Urassa kutoka kampuni ya Estim, ambao ndio waliokuwa na kandarasi ya kufunga taa hizo, amesema  wanaamini taa hizo zitakuwa mwarobaini wa watumiaji kupita kwa usalama bila kuathirika kwa kugongwa.

 “Tunaishukuru sana serikali kupitia TANROADS kwa kutuamini katika kazi hii ya kuweka taa tumeifanya vizuri, tunafanya pia kazi ya ujenzi wa barabara, madaraja na makalavati, na tunaahidi kuendelea na ushirikiano na serikali katika kufanya kazi bora na zenye viwango,” amesema Mhandisi Leonard.