News

NAIBU WAZIRI KWANDIKWA AAGIZA UKARABATI DOM – MORO KUKAMILIKA HARAKA.

Na Siti Said

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi wa kampuni CGI Contractors Limited anayekarabati barabara ya Dodoma- Morogoro sehemu ya Magubike na Gairo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo mapema ili kupunguza adha ya msongamano wa magari katika eneo hilo.

Agizo hilo amelitoa leo wilayani Gairo mkoani Morogoro akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu inayosimamiwa na sekta yake katika mikoa ya Dodoma na Morogoro ili kujionea maendeleo yake.

Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa amemsisitiza mkandarasi huyo kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakuwa imara hususan katika sehemu za miinuko ili kuzuia ajali zinazoweza kutokea katika maeneo hayo.

"Hakikisheni mnamaliza haraka ukarabati wa barabara hii, magari hapa yamekuwa mengi na msongamano ni mkubwa, mnachotakiwa kufanya kwa sasa ni kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili muweze kukabiliana na mvua na huku mkipanga ratiba zenu kuhakikisha mnakamilisha kazi hii mapema", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Akiwa njiani kuelekea mkoani Morogoro katika eneo la Kibaigwa (panda mbili) mjini Dodoma, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua madaraja yanayojengwa na Wakala wa Barabara ( TANROADS), mkoani humo na kuwapongeza kwa ujenzi wa madaraja hayo ili kudhibiti maji yanayotuama hapo hususan katika kipindi cha mvua na kusababisha kero kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa barabara ya Dodoma - Morogoro kutokana na mahitaji ya barabara hiyo kuonekana kuwa ni makubwa kutokana na ongezeko la watu na magari mara baada ya Serikali kuhamia Dodoma.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua maendeleo ya ujenzi katika mradi wa mizani eneo la Dakawa Magereza ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa amefurahishwa na ujenzi wake kwa kuwa ni wa kisasa.

"Matumaini yangu ni kuwa hatutashuhudia foleni hapa na watumiaji wa mzani  huu hawatatumia muda mwingi kupata huduma pindi mradi utakapokamilika kutokana na ujenzi wake kuwa ni wa kisasa", amesisitiza Naibu Waziri.

Amemtaka mkandarasi anayejenga mzani huo kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo kwa wakati na kuwezesha mizani hiyo kuanza kutoa huduma mapema.

Amefafanua kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha   inajenga mizani kubwa nyingi na za kisasa nchini ambazo zitakidhi mahitaji ya watumiaji ikiwemo kuwa na sehemu ya kutolea mafunzo kwa madereva, sehemu ya kupumzika na  kuweka mizigo.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Morogoro, Mhandisi Dorothy Mtenga, amesema kuwa mradi huo umefika asilimia 70  na  kazi zinazofanyika kwa sasa ni kutengeneza barabara ya lami, barabara za zege na kuweka taa za barabarani.

Amesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa mizani mbili za kisasa za kupima magari ambao unafadhiliwa na Serikali  kwa asilimia mia moja unagharimu jumla ya shilingi Bilioni 14.784 na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwakani.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,

Uchukuzi na Mawasiliano.