“WAKATI WA WAHANDISI WAZAWA NI SASA” - KAIMU MTENDAJI MKUU WA TANROADS, MHA. EPHATAR MLAVI
Dar es Salaam, 23 Februari 2026
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Ephatar Mlavi, amewasha moto wa matumaini na kujiamini kwa wahandisi vijana, akisisitiza kuwa zama za wataalamu wa Kitanzania kuwa watazamaji zimekwisha sasa ni wakati wa kuongoza.
Akizungumza na wanafunzi wa Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET) katika University of Dar es Salaam, Mlavi alizungumza kwa msisitizo na uwazi kuhusu mustakabali wa sekta ya ujenzi nchini.
Alikiri kuwa bado kuna pengo kati ya ushiriki wa wazawa na makampuni ya kigeni katika miradi mikubwa, lakini akaweka wazi kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi kubadili hali hiyo.
Alieleza kuwa kila mradi mkubwa unaotekelezwa nchini unapaswa kuwa darasa la vitendo kwa wahandisi wazawa kupitia ushiriki wa wakandarasi wasaidizi (sub-contractors), ili kuwajengea uzoefu, uthubutu na uwezo wa kusimamia miradi mikubwa kwa viwango vya kimataifa.
“Tunataka wahandisi wa Kitanzania wasimame mbele, si pembeni. Miradi hii ni yao, taifa hili ni lao,” amesisitiza Mhandisi Mlavi kwa kujiamini.
... Kwa msisitizo zaidi, amekumbusha kuwa Serikali imetenga asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalum, hususan vijana, ikiwa ni fursa ya kipekee ya kujenga kizazi kipya cha wataalamu watakaoongoza mageuzi ya miundombinu ya taifa.
Mhandisi Mlavi aliwahamasisha wanafunzi kuacha kusubiri ajira bali wajitayarishe kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa, akiahidi kuwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) iko tayari kuwakaribisha, kuwafundisha na kuwapa nafasi ya kuthibitisha uwezo wao.Hotuba yake haikuwa tu ya kitaaluma, bali ya kuamsha ari, uzalendo na kujiamini.
Ujumbe wake ulikuwa mmoja na wazi - wahandisi wa Kitanzania wana kila sababu ya kuamini katika uwezo wao, kwa sababu wakati wao wa kung’ara ni sasa.