News

MHANDISI NYAMHANGA AAGIZA MKANDARASI KURUDI ENEO LA KAZI

Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, ameagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kumuandikia barua mkandarasi wa Kampuni ya Impesa di Construzioni anayejenga kituo cha ukaguzi wa pamoja (one stop inspection station) eneo la Manyoni mkoani Singida na Nyakanazi mkoani Kagera kurejea eneo la kazi na kuendelea na ujenzi. 

 

Akizungumza katika kijiji cha Muhalala mkoani Singida wakati wa ukaguzi wa kituo hicho, Katibu Mkuu huyo amesema Serikali tayari imeshashughulikia madai ya mkandarasi huyo, hivyo hana sababu ya kutoendelea na ujenzi wa mradi huo. 

 

"Naagiza Mkandarasi huyu arudi eneo lake la kazi na kuanza kazi ya ujenzi wa mradi huu mara moja", amesema Mhandisi Nyamhanga.

 

Aidha, Mhandisi Nyamhanga, ameeleza kuwa jumla ya gharama za mradi wa vituo hivyo ni takribani shilingi bilioni 55, ambayo itahusisha gharama za ujenzi, usimamizi na fidia.

 

Mhandisi Nyamhanga amefafanua kuwa ujenzi wa kituo hicho unaenda sambamba na ujenzi wa kituo kingine eneo la Nyakanazi mkoani Kagera ambapo kituo kingine cha vigwaza mkoani Pwani kimeshakamilika na hivyo kutafanya jumla ya vituo vikuu vitatu vya ukaguzi vyenye umbali wa kilomita 500 kutoka kwa kila kimoja.

 

Amefafanua kuwa lengo la ujenzi wa mizani hizo ni kupunguza vizuizi barabarani na gharama za usafirishaji wa mizigo kupitia barabara ya ukanda wa kati.

 

Kwa sasa magari ya mizigo husimama takriban katika vituo 31 ambapo kati ya hivyo vituo nane ni vya mizani, vituo 20 ni vya polisi na vituo 3 ni vya ukaguzi wa mapato ambavyo vyote viko kati ya Dar es Salaam hadi mipaka ya Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa umbali wa kilomita 1000.

 

Awali, akitoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, Kaimu Meneja wa TANROADS  mkoa wa Singida Mhandisi Masige Matari, amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 60 na kazi zinazoendelea kutekelezwa ni kama vile barabara zinazoingia na kutoka kituoni.

 

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Chaya hadi Nyahua mkoani Tabora yenye urefu wa KM 85.4 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi CHICO, ambapo ameridhishwa na maendeleo yake na kumtaka mkandarasi huyo kufanya kazi kwa bidii ili mradi huo ukamilike mapema zaidi ili kufungua mkoa huo kwa fursa za kibiashara na usafirishaji wa abiria na mizigo.

Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa Tabora Mhandisi Damian Ndabalinze, amemuhakikishia Katibu Mkuu huyo kuusimamia kwa ukamilifu mradi huo na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa mkoani humo.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait (KFAED) na kukamilika kwake kutafungua mkoa wa Tabora na mikoa ya Katavi na Kigoma katika kukuza uchumi wa wananchi.

Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Nyamhanga, yupo katika ziara ya kikazi mkoani Tabora  ikiwa ni lengo la kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na sekta yake hususani barabara, madaraja na kiwanja cha ndege.

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano