WAZIRI MKUU AWATAKA WANANCHI SAME KUTUNZA MIUNDOMBINU
Kilimanjaro, 18 Februari, 2026
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa Same kutunza miundombinu inayojengwa na Serikali kwa manufaa yao.
Amesema hayo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Same- Ndungu- Mkomazi yenye kilometa 105, katika sehemu Mkomazi -Ndungu Km 36 ambayo ujenzi wake unaendelea.
"Wizara ya Ujenzi hakikisheni ujenzi wa barabara hii ya kimkakati unakamilika kwa viwango na kuchochea ukuaji wa shughuli za kilimo, uvuvi na utalii," amesisitiza Waziri Mkuu Mhe. Nchemba.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara hiyo umegawanywa katika sehemu tatu ili kurahisisha ujenzi wake ambazo ni Gonja-Ndungu yenye Km. 5.2; Ndungu-Mkomazi yenye Km 36 na Same- Mroyo Km 56.8.
Mhandisi Kasekenya amebainisha kuwa katika kuiunganisha vizuri Wilaya ya Same kwa barabara za lami, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Ndungu-Miamba-Mwembe yenye Km 90, ili kuijenga kwa kiwango cha lami na hivyo kurahisisha usafiri kati ya maeneo ya milimani na tambarare.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Jefferson Nnko amesema wamejipanga kuhakikisha ujenzi wa barabara hizo unakamilika kwa ubora uliosanifiwa.
Waziri Mkuu Nchemba yuko katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Kilimanjaro kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.