NIMERIDHISHWA NA KASI YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA UJENZI WA BARABARA KUTOKA BAGAMOYO - MKANGE - TANGA - PANGANI
ULIOGHARIMU KIASI CHA SHILINGI BILIONI 317.6
Pwani, 15 Februari, 2026
Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba amesema serikali imeridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Bagamoyo kupitia Mkange kwenda Tanga hadi Pangani yenye urefu wa Kilometa 256 na kusema kuwa serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara katika ngazi zote ili kuongeza kasi ya maendeleo.
Akiwahutubia wananchi waliofika kumlaki wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika daraja jipya la mto Pangani, Dkt Mwigulu amesema ujenzi wa barabara zenye miundombinu ya kisasa ni jambo ambalo serikali imelipa kipaumbele na kuiagiaza Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kuweka miundombinu inayoendana na kasi ya ukuaji wa mji huo.
" Binafsi nawapongeza sana kwa kazi nzuri iliyotokana na usimamizi makini wa mradi huu, siku za nyuma tulizoea kuona madaraja kama haya katika nchi za wenzetu, lakini leo hii tunashudia imewezekana kufanyika hapa Pangani, shilingi bilioni 317 zimewaokoa maelfu ya Wanatanga" alisema Dkt Mwigulu.
Aidha Dkt Mwigulu ameongeza kuwa serikali itahakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wadau wote wa maendeleo ikiwemo wafanyabiashara ili kuhakikisha mazingira ya uwekezaji uliofanyika yanaendana na mahitaji ya eneo husika ikiwa ni pamoja na kuongeza maeneo ya maegesho ya magari pamoja na ukubwa wa stendi ya mabasi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt Batilda Buriani amemshukuru Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuupa kipaumbele mkoa wa Tanga katika ujenzi wa miundombinu ya barabara hatua ambayo amesema itachangia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi katika mkoa huo.