News

BARABARA ZA KISASA KUONGEZEKA NCHINI

Imeelezwa kuwa ujenzi na usimamizi bora wa barabara za kisasa katika miji mikuu utachochea kukua kwa haraka kwa uchumi na kuvutia biashara za bidhaa na utalii hapa nchini.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema hayo jijini Arusha leo, wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa  uliondaliwa na Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC), na Wizara yake unaohusu mapinduzi ya sekta ya usafirishaji na mabadiliko ya kiuchumi katika nchi zinazoendelea na kusisitiza kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kutenga bajeti inayokidhi ili kutekeleza miradi ya ujenzi na usafirishaji hapa nchini.

Aidha, amewataka watalaam wa Wizara na Taasisi zake kushiriki kikamilifu, kujifunza ili kupata utaalam na uzoefu kutoka nchi zilizoendelea katika sekta ya miundombinu ya barabara na usafirishaji.

"Tumejipanga kuhakikisha tunakuwa na barabara bora zinazoweza kupitika wakati wote na zinazounganisha nchi yetu na nchi jirani ili kuvutia huduma za biashara, masoko, kilimo na viwanda ifikapo 2025", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.

Mkutano huo wa kimataifa unaoongozwa na kauli mbiu isemayo "Mapinduzi ya Nne ya Sekta ya Usafirishaji" unahudhuriwa na wadau zaidi ya 200 kutoka nchi 25 duniani unawaweka pamoja wadau wa barabara kubadilishana uzoefu na teknolojia mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya barabara na usafirishaji miongoni mwa nchi wanachama.

Nchi zinazohudhuria mkutano huo ni Bangladesh, Botswana, Canada, Jamhuri ya Czech, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Ufaransa, Ujerumani, Ghana na Japan.

Nyingine ni Kenya, Liberia, Madagaska, Msumbiji, Nepal, New Zealand, Nigeria, Rwanda, Seirra Leone, Afrika Kusini, Korea kusini, Sudan Kusini, Sri Lanka, Uturuki, Uganda, Uingereza na mwenyeji Tanzania.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo utaangalia matokeo ya uwekezaji katika miundomibinu ya usafirishaji na kujadili kwa undani changamoto zinazokabili nchi zinazoendelea ikiwemo  ufinyu wa rasilimali za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na uboreshaji wa huduma nyingine za kijamii kama maji, afya, elimu na nishati kwa wakati mmoja.

Shirikisho la Barabara Duniani (PIARC), lenye nchi wanachama 121 lilianzishwa mwaka 1909 na Tanzania ilijiunga mwaka 1992 ambapo mwaka huu Chama cha Barabara (TARA), kimeteuliwa kuwa mwakilishi wa Kamati ya Kitaifa ya PIARC hatua itakayoongeza fursa za uzoefu na teknolojia kwa Tanzania.

Mkutano huo uliofunguliwa rasmi leo unawakutanisha wataalam wa masuala ya barabara na teknolojia utafungwa kesho ambapo zaidi ya washiriki 200 wanahudhuria.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano