News

WAZIRI KAMWELWE KUFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA WA WADAU WA BARABARA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, anatarajiwa kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu mapinduzi ya sekta ya usafirishaji na mabadiliko ya kiuchumi katika nchi zinazoendelea, jijini Arusha.

Mkutano huo wa siku mbili (2) ulioandaliwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kushirikiana na Shirikisho la Barabara Duniani (World Road Association-PIARC), utafanyika katika ukumbi wa kimataifa wa AICC.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema maandalizi kwa ajili ya mkutano huo yamekamilika ambapo takribani washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi 25 duniani watashiriki mkutano huo.

Mkutano huo ambao lengo lake kuu ni kuangalia matokeo ya uwekekezaji katika mundombinu ya usafirishaji utajadili kwa kina mada mbalimbali zinazohusu changamoto zinazozikabili nchi zinazoendelea ikiwemo rasilimali chache za kuimarisha miundimbinu ya usafirishaji wakati huohuo kuboresha huduma nyingine za kijamii kama vile maji, afya, elimu na nishati.

"Tutajadili namna ya kuimarisha miundombinu ya kisasa ya usafiri na usafirishaji inayoendana na teknolojia inayopatikana katika nchi zinazoendelea", amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Barabara Tanzania (TARA), Bw. Joseph Haule, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano huo amezitaja nchi zitazoshiriki kuwa ni Bangladesh, Botswana, Canada, Jamhuri ya Czech, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Ufaransa, Ujerumani, Ghana na Japan.

Nyingine ni Kenya, Liberia, Madagaska, Msumbiji, Nepal, New Zealand, Nigeria, Rwanda, Seirra Leone, Afrika Kusini, Korea kusini, Sudan Kusini, Sri Lanka, Uturuki,Uganda, Uingereza na mwenyeji Tanzania.

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa PIARC. Bw. Patrick Mallejacq, amesema kufanyika kwa mkutano huo Tanzania kutafungua fursa za kiuchumi, kijamii na kiteknolojia  katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Tanzania ilijiunga na PIARC mwaka 1992 na mwaka huu TARA imekubaliwa kuwa kamati ya kitaifa ya PIARC katika mkutano uliofanyika Yokohama nchini Japani mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2018.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano