News

ELIMU YA UTHAMINI YATOLEWA SAMBAMBA NA UUNDAJI WA KAMATI ZA MALALAMIKO YA FIDIA SWAYA

ELIMU YA UTHAMINI YATOLEWA SAMBAMBA NA UUNDAJI WA KAMATI ZA MALALAMIKO YA FIDIA SWAYA

Mbeya

24/01/2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea na zoezi la kuunda Kamati za Kusikiliza Malalamiko yanayotokana na fidia kwa wananchi waliopitiwa na mradi wa barabara ya mchepuo ya Uyole kwenda Songwe, ambapo safari hii zoezi hilo limefanyika katika Kata ya Swaya mkoani Mbeya.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mthamini Mwandamizi kutoka TANROADS Makao Makuu, Anna Deo Urassa, amesema uundaji wa kamati hizo unalenga kutoa fursa kwa wananchi kuwasilisha malalamiko yao endapo hawajaridhika na viwango vya fidia walivyolipwa, kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa ujenzi wa mradi.

Urassa amesema katika kata hiyo tayari baadhi ya wananchi waliolipwa fidia wameanza kuondoa mali zao ikiwemo nyumba na mabati, huku wengine wakianza taratibu za kubomoa, hali inayoashiria maandalizi mazuri ya utekelezaji wa mradi huo.

Amefafanua kuwa katika zoezi la uthamini, alama za kijani huwekwa kwa wananchi ambao mali zao zimeguswa na usanifu wa barabara na hivyo wanastahili kulipwa fidia, wakati alama za rangi nyekundu huashiria wale waliovamia eneo la hifadhi ya barabara na ambao hawastahili fidia kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Urassa ameongeza kuwa kupitia kamati za malalamiko, mwananchi anayehisi kutoridhika na fidia aliyopata anapewa nafasi ya kuwasilisha malalamiko yake, ambapo wataalam wa uthamini wanaweza kurejea tena kukagua mali husika ili kujiridhisha zaidi kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Kwa upande wake, Mthamini wa TANROADS, Saad Athuman, amesema ziara yao imelenga kufuatilia utekelezaji wa makubaliano baada ya ulipaji wa fidia, ambapo wamejionea baadhi ya wananchi wakiondoa mali zao na kuhamia maeneo mengine, jambo linaloonesha uelewa wa taratibu za mradi.

Katika hatua nyingine Athuman ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za fidia, hatua iliyosaidia wananchi kuanza kuondoka katika maeneo yaliyopitiwa na mradi na kuweka mazingira wezeshi ya kuanza kwa utekelezaji wa barabara ya mchepuo kwa manufaa ya Mbeya na Taifa kwa ujumla.