News

WAZIRI KAMWELWE AMTAKA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI WA BARABARA MAPEMA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amemtaka mkandarasi wa kampuni ya China Henan International Cooperation (CHICO), anayejenga barabara ya Nyahua –Chaya yenye urefu wa KM 85.4 kukamilisha barabara hiyo ifikapo mwezi Desemba 2020 badala ya Machi 2021.

Amezungumza hayo mkoani Tabora, wakati akikagua hatua za maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 117.9 na kuridhishwa na ubora wa kazi zilizoanza kutekelezwa.

Amemtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi  ambao umefikia asilimia 12 ikiwa ni nyuma ya mpango kazi kwa asilimia 4.

Waziri Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Kuwait (KFAED) na kukamilika kwake kutafungua mkoa wa Tabora na mikoa ya Katavi na Kigoma katika kukuza uchumi wa wananchi.

Waziri Mhandisi Kamwelwe, amefafanua kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu katika kukuza biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo ikiwemo inayokwenda nchi jirani.

Aidha, Waziri Kamwele ameonesha kusikitishwa kwa vitendo vya baadhi ya wananchi kuhujumu miundombinu ya barabara ikiwemo alama za barabarani hasa katika mkoa huo na kuomba kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kusaidia Serikali katika kudhibiti.

"Kuna watu huku Tabora waliokamatwa na vyuma vya alama za barabarani majumbani mwao wakitwangia mahindi, hili suala halikubaliki na yeyote atakayepatikana sheria kali zitachukuliwa dhidi yake na Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi zaidi ili kudhibiti suala hili", amefafanua Waziri Kamwelwe.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Tabora Mhandisi Damian Ndabalinze, amemueleza Waziri huyo kuwa ujenzi wa barabara hiyo utahusisha ujenzi wa madaraja makubwa mawili, makalvati yenye pembe nne 32 na makalvati ya mduara 60.

Akizungumzia changamoto za mradi, Mhandisi Ndabalinze amemueleza Waziri kuwa sehemu ya mwanzo ya mradi yenye urefu wa KM 1.7 ipo kwenye bonde ambalo kwa kipindi cha mvua za mwaka huu lilifurika kwa zaidi ya siku saba na kusababisha kufunga barabara hiyo ambapo eneo hilo sasa linajengewa makalvati ya pembe nne yasiyopungua saba na kujazwa mawe kwa zaidi ya mita moja juu ya tabaka la mchanga.

Waziri Mhandisi Kamwelwe yupo katika ziara yake ya siku tatu mkoani Tabora ikiwa ni lengo la kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea mkoani humo