News

MKUU WA MKOA WA KUSINI UNGUJA AIPONGEZA TANROADS

MKUU WA MKOA WA KUSINI UNGUJA AIPONGEZA TANROADS

Zanzibar, 14 Januari, 2026

Mkuu wa mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar Mhe. Hamida Khamis.ameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kujenga miundombinu mbalimbali.

Mhe. Hamida amesema hayo wakati alipotembelea banda la maonesho ya 12 ya Biashara ya Kimataifa ya Zanzibar (ZITF) yanayofanyika Fumba, Dimani.

“Tunapongeza sana na nyie ni wanawake nawaona hapa na nimesikia hapa wengine ni wahandisi mpo mbele tunajivunia kwa utendaji wa kazi za ujenzi mnazozifanya,” amesema Mhe. Hamida.

Pia amesema kwa Zanzibar wamejenga daraja Kisiwa cha Uzi Km 2.2, ambapo awali maji yalikuwa yakijaa na kusababisha watu kushindwa kupita.

Pia amesema kutakuwa na mradi mkubwa wa kujenga daraja la kuwaunganisha Kaskazini na Kusini Unguja litakaloanza kujengwa eneo la Charawe - Chwaka.

Kwa upande wake, Meneja wa Mazingira na Jamii, Bi. Zafarani Madayi amesema TANROADS kwenye maonesho hayo inatoa elimu mbalimbali kwa wananchi wanaotembelea banda lao la maonesho.

Bi. Zafarani amesema TANROADS inakazi ya kujenga barabara, madaraja na viwanja vya ndege na kuhusimamia vituo vya mizani iliyopo kwenye kila mkoa.

“Kwa sasa mtandao wa barabara ni zaidi ya Km. 37,435, na tumeweza kujenga madaraja ya kimkakati likiwemo la JPM lililopo Mwanza, Tanzanite, Mfugale na Kijazi haya yote yapo Dar es Salaam; lakini pia tumejenga viwanja vya ndege kikiwemo cha Songwe, na sasa tunaendelea na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, Dodoma,” amesema Bi. Zafarani.

Hatahivyo, amesema katika ujenzi wa barabara TANROADS inazingatia usalama pamoja na masuala ya mazingira kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ili kuona athari kwa jamii na kuona faida na hasara za mradi.

Amesema pia wanasimamia mizani 83 kwa kudhibiti wasafirishaji wa magari makubwa ya mizigo, ili kuhakikisha barabara zinadumu kwa muda mrefu.