DARAJA LA LUFILYO LAPOKELEWA RASMI BAADA YA KUKIDHI VIWANGO VYA KITAALAMU
Njombe.
10, January 2026
Mhandisi Mkuu wa Kitengo cha Ushauri wa Kihandisi cha Wakala ya Barabara Tanzania (TECU), Mhandisi Lutengano Mwandambo, amekagua na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Daraja la Lufilyo na kulipokea rasmi kutoka TECU Mkoa wa Njombe baada ya kubaini kuwa kazi imefanyika kwa viwango vinavyokubalika kitaalamu.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi huo, Mhandisi Mwandambo alisema daraja la Lufilyo ni moja ya miradi ya dharura iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia kufuatia madhara ya mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya, na kwamba utekelezaji wake umefanyika kwa ubora uliokusudiwa.
Aliongeza kuwa mkandarasi alifanya kazi kwa bidii usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa. Alibainisha kuwa daraja limekamilika, taa za barabarani zimefungwa na barabara za maingilio tayari zimekamilishwa.
Kwa upande wake Emanuel Tang'ale Ambae ni mhandisi wa wa mradi huo kutoka Makao makuu ya TANROADS alisema daraja lina urefu wa mita 40 na barabara za maingilio zenye jumla ya urefu wa kilometa 3.1, huku vifurushi (package) vyote vya mradi vikikamilika.
Alisema mradi mzima umegharimu shilingi bilioni 6 na ulitekelezwa na kampuni ya China Aero National Engineering Cooperation,kutoka nchini China. Alibainisha kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutafungua lango la kiuchumi kati ya Mkoa wa Njombe na Mbeya, na kurahisisha usafirishaji wa watu na mazao.
Nae Mhandisi wa Madaraja katika Mradi huo Japhet Meta alisema, utekelezaji wa mradi ulianza Januari 3, 2025 na kwa sasa umefikia mwisho wa utekelezaji wake licha ya changamoto walizokumbana nazo katika utekelezaji wake, na Mkandarasi anamalizia Kazi ndogo za ulinzi wa miundombinu ( protection works) ambazo haziathiri matumizi ya daraja hilo kwasasa.
Kwa upande wa wananchi, Bwana Alphonce Mwambopo,Mkazi wa Kijiji Kikuba alisema kabla ya ujenzi wa daraja hilo, kulikuwepo na madaraja madogo madogo yaliyokuwa yanabomoka mara kwa mara na kusababisha vifo na ajali kwa watumiaji wa barabara hiyo .
Wananchi wa Lufilyo waliahidi kushirikiana na Serikali katika kuutunza mradi huo na miundombinu yake yote, ikiwemo taa za barabarani, ili kuhakikisha unadumu na kuendelea kuleta maendeleo kwa muda mrefu.