TANROADS NA ZANROADS WASHIRIKIANA KUTOA ELIMU ZITF
Zanzibar, 10 Januari, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na Wakala ya Barabara Zanzibar (ZANROADS) wanaendelea kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi wanaotembelea banda lao katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara (ZITF) yanayoendelea katika eneo la Dimani–Fumba, Zanzibar.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa ZANROADS, Mhandisi Safia Juma Ameir, amesema kuwa katika banda hilo wanatoa elimu mbalimbali, ikiwemo matumizi ya alama za uvamizi wa maeneo ya barabara.
Mhandisi Safia amesema kuwa kwa sasa wananchi wengi, ama kwa kutokujua au kwa makusudi, wamekuwa wakiondoa alama zinazowakataza kujenga nyumba za makazi au kufanya shughuli nyingine za kibiashara katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara.
“Wapo waliolipwa fidia na kuondoshwa ili ujenzi uanze, lakini wamekuwa wakirudi tena kuanza ujenzi upya. Sasa tumekuja na utaratibu wa kuweka nguzo ili kuzuia uvamizi, na watakaokaidi watachukuliwa hatua kali,” amesisitiza Mhandisi Safia.
Ameongeza kuwa Zanzibar inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ya ujenzi, ikiwemo madaraja ya juu katika maeneo ya Mwanakwerekwe na Amani. Aidha, kutakuwa na ujenzi wa madaraja ya Mkokotoni–Tumbatu na Chwaka, ambayo yatajengwa kwa utaratibu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi (PPP).
Pia amesema kuwa daraja linalounganisha Kisiwa cha Uzi tayari limekamilika, huku kazi nyingine mbalimbali za ujenzi zikiendelea.