News

MADARAJA YA LOSINYAI NA MINJINGU KUWA MKOMBOZI KWA MKOA WA MANYARA

MADARAJA YA LOSINYAI NA MINJINGU KUWA MKOMBOZI KWA MKOA WA MANYARA

Manyara, 20 Desemba 2025

Madaraja ya Losinyai na Minjingu yanayoendelea kujengwa mkoani Manyara yakikamilika yataongeza usafiri salama na kuinua shughuli za kiuchumi kwa wakazi na watumiaji wa barabara hiyo, imeelezwa.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo iliyo chini ya utaratibu wa miradi ya dharura (CERC), Mhandisi Nchama Wambura wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS amesema miradi hiyo itawawezesha wananchi kusafirisha mazao ya biashara kwa uhakika na kufika maeneo mbalimbali kwa urahisi. Mkoa wa Manyara una miradi mitano ya CERC. 

Mhandisi Wambura ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi hiyo ambayo itanufaisha watumiaji wa madaraja na barabara kuu ya Manyara–Arusha pamoja na mikoa ya Singida, Dodoma na Kilimanjaro.

Amesema awali wananchi walikuwa na wasiwasi kuvuka hasa kipindi cha mvua kutokana na daraja la zamani kujaa maji, lakini sasa daraja jipya lililoinuliwa litaondoa changamoto ya mafuriko.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkaazi wa TANROADS Mkoa wa Manyara, Mhandisi Charles Lyamuya amesema daraja la Losinyai lina urefu wa mita 80 na lina midomo minne, kila mmoja ukiwa na upana wa mita 20. 

Amesema kazi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa kingo na kuta, na linatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Desemba 2025.

Amesema daraja la Minjingu lenye urefu wa mita 50 limekamilika kwa asilimia 99.5, ambapo kwa sasa wanaendelea kuweka alama za barabarani na kufanya usafi wa mazingira kabla ya kuanza kutumika, pamoja na kuondoa daraja la zamani ili kuruhusu maji kupita vizuri wakati wa mvua. Madaraja yote mawili yanatarajiwa kukamilika mwezi Desemba.

Mhandisi Lyamuya ameongeza kuwa miradi mingine mitatu ya CERC iliyokamilika ni daraja la Katesh pamoja na maboksi makalavati mawili ya Msasani na Dabil. Miradi hiyo inatekelezwa na Mkandarasi mzawa, Kampuni ya Rocktronic ya Jijini Moshi.