News

WAZIRI KAMWELWE AAGIZA TANROADS KUICHUNGUZA KAMPUNI YA CHICO

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Njombe kumchunguza mkandarasi wa Kampuni ya China Henan International Cooperation (CHICO), anayejenga barabara ya Njombe-Moronga yenye urefu wa KM 53.9 kwa kiwango cha lami kama ana wataalaamu wa kutosha.

Waziri Mhandisi Kamwelwe ametoa agizo hilo katika wilaya ya Wanging'ombe mara baada ya kukagua hatua zilizofikiwa katika mradi huo na kutoridhishwa na kasi  ya ujenzi wake ambapo mpaka sasa umefikiwa kwa asilimia 14.

Mhandisi Kamwelwe amesema hana uhakika na kampuni hiyo kama ni  wenyewe CHICO waliozoeleka katika uendeshaji wa miradi mingi hapa nchini hasa ya barabara.

"Sijaridhishwa na kasi ya huu ujenzi, Meneja wa TANROADS hakikisha unafuatilia kwa makini mradi huu na kubaini sababu zilizopelekea kusuasua kwa mradi na kuondoa wataalamu ambao wataonekana wanaudhaifu na kukwamisha mradi huo", amesisitiza Mhandisi Kamwelwe.

Amebainisha kuwa  hakuna sababu ya mkandarasi huyo kuchelewesha mradi huo kwani vifaa na mitambo yote ipo katika eneo la kazi na tayari Serikali imeshamlipa fedha alizozidai kwa asilimia 95.

Aidha, amemueleza Mkandarasi wa Kampuni ya CHICO kuwa Serikali haitamuongezea muda wa kuikamilisha barabara hiyo na wananchi wanaiongojea kwa hamu kubwa kwani Serikali imewaahidi wananchi hao ambao toka Uhuru hawajawahi kuiona lami.

Katika hatua nyingine, Waziri Kamwelwe amekagua ujenzi wa mradi wa barabara ya Moronga-Makete yenye urefu wa KM 53.5 inayojengwa na mkandarasi kutoka kampuni ya China Railway Seventh Group na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake.

Awali akitoa taarifa Meneja wa TANROADS, mkoa wa Njombe, Mhandisi Yusuph Mazana, amemueleza Waziri Mhandisi Kamwelwe changamoto ya miradi hiyo kubwa ni kazi za ujenzi kuanza katika msimu wa mvua nyingi na hivyo kupunguza kasi ya ujenzi wake.

Pia amemuahidi Waziri huyo kuwasimamia makandarasi hao katika kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na viwango vya ubora.

Naye Mbunge wa jimbo la Wanging'ombe, Gerson Lwenge, ameishukuru Serikali kwa hatua ya ujenzi wa barabara ya Njombe-Moronga kwani ni muhimu katika usafirishaji wa mazao ya misitu na viazi.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete yenye jumla ya urefu wa KM 107.4 unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na unatarajiwa kukamilika Januari 2020.