News

MKUU WA WILAYA YA ARUSHA  AIPONGEZA TANROADS KUWA KIDIGITALI

MKUU WA WILAYA YA ARUSHA  AIPONGEZA TANROADS KUWA KIDIGITALI

Arusha,  17 Desemba, 2025

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude ameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kwa kutumia mfumo wa udhibiti wa ubora wa barabara unaoendeshwa kidigitali.

Mhe. Mkude ameyasema hayo wakati alipotembelea banda la maonesho la TANROADS yaliyokwenda sambamba na mkutano wa 18 Kutathmini Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi, unaowakutanisha Serikali, wadau wa maendeleo, wadhibiti, waendeshaji na sekta binafsi uliofanyika Jijini Arusha hivi karibu.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha apongeza TANROADS kuwa mtambo mzuri unaoendeshwa kidigitali.Hatahivyo, amewataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuujenga uchumi wa taifa, ambapo wananchi wataelewa utekelezaji wa miradi mikubwa nchini.

Awali akimkaribisha Mhe. mkuu wa wilaya, Mhandisi wa Miradi kutoka TANROADS, Cecilia Kalangi alisema mtandao wa barabara umeongezeka kutoka Km. 4000 hadi kufikia Km. 12,000.

Pia Mhandisi Cecilia amesema mwaka 2017 TANROADS ilikasimiwa ujenzi wa viwanja vya ndege, ambapo tayari viwanja kadhaa vimeshakamilika na vingine vipo katika hatua nzuri ya kukamilika kikiwepo Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kilichopo Dodoma.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Majenzi kutoka kitengo cha Utafiti cha TANROADS, Maxmilian Mwapule amesema mtambo wa kukagua ubora wa barabara umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara, ambapo unatumia mfumo wa mionzi inayokwenda chini ya ardhi na kurudisha matokeo ya hali halisi ya eneo la barabara lililokuwa likipimwa.

Wakati huo huo TANROADS imepata tuzo kwenye mkutano huo kutokana na jitihada zake katika ujenzi wa miundombinu.