Mafunzo ya Usimamizi wa Ujenzi TANROADS Yaimarisha Afya ya Akili
Arusha, 17 Desemba, 2025
Washiriki wa mafunzo ya Usimamizi wa Ujenzi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) wamepata fursa ya kujifunza kwa vitendo na kuimarisha mshikamano pamoja na afya ya akili kupitia ziara ya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, mkoani Arusha.
Ziara hiyo ni sehemu ya mafunzo yenye lengo la kuwajengea washiriki uelewa mpana unaochangia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara, sambamba na kuunga mkono jitihada za Kitaifa za kukuza utalii wa ndani.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Mhandisi Frank Mwakisonga amesema ziara hiyo imelenga kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, huku ikichangia moja kwa moja pato la Taifa.
“Mbali na kuongeza uelewa na mshikamano miongoni mwa washiriki wa mafunzo, ziara hii imesaidia kuboresha afya ya akili kwa kuondoa msongo wa mawazo, jambo ambalo lina mchango mkubwa katika kuongeza tija na ufanisi kazini,” amesema Mhandisi Mwakisonga.
Ameongeza kuwa viongozi na watumishi wa umma wana wajibu wa kuwa mabalozi wa utalii wa ndani kwa vitendo, hatua inayosaidia kukuza uchumi wa Taifa na kulinda rasilimali za asili.
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara wa kutangaza vivutio vya utalii wa Tanzania kimataifa kupitia filamu ya The Royal Tour inayorushwa duniani kote, hivyo ushiriki wa taasisi za umma katika utalii wa ndani ni utekelezaji wa maono hayo kwa vitendo.
Kwa TANROADS, mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa kitaalamu, kujenga morali ya watumishi na hatimaye kuchangia utekelezaji bora wa miradi ya miundombinu inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa.