MADARAJA SABA YA KIMKAKATI YATOA SULUHU YA FOLENI: TANROADS YAWEKA MIKAKATI YA MUDA MREFU DAR ES SALAAM
Arusha, 16 Desemba, 2025
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umeweka mikakati ya muda mrefu ya kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam kwa ujenzi wa madaraja ya juu, yakijumuisha madaraja saba ya kimkakati miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa.
Akitoa wasilisho la maendeleo ya taasisi kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita katika Mkutano wa 18 wa Kutathmini Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi, unaowakutanisha Serikali, wadau wa maendeleo, wadhibiti, waendeshaji na sekta binafsi unaofanyika Jijini Arusha, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu, Mhandisi Ephatar Mlavi, akimwakilisha Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema TANROADS inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa madaraja 10 ya juu, ambapo baadhi yamekamilika na mengine yapo katika mpango wa kujengwa.
Mhandisi Mlavi ameyataja madaraja yaliyokamilika kuwa ni Kijazi (Ubungo), Mfugale (Tazara), Tanzanite na Kurasini, huku miradi inayotarajiwa kujengwa ikijumuisha Jangwani, Morocco, Kigamboni, Kongowe, Mwenge, pamoja na barabara ya mzunguko na kituo cha kutoa huduma cha pamoja.
Amesema kwa sasa hali ya barabara nchini ni nzuri, ambapo takribani asilimia 90 ya mtandao wa barabara zinapitika vizuri, huku miradi yote ikitekelezwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za mazingira, kama ilivyokubaliwa katika sekta.
“Hali ya barabara kwa sasa ni nzuri; asilimia 90 zinapitika vizuri, na miradi yote inatekelezwa kwa kuzingatia sheria za mazingira,” amesema Mhandisi Mlavi.
Aidha, amesema TANROADS imepiga hatua kubwa kwa kuongeza mtandao wa barabara za kiwango cha lami hadi kufikia takribani Km 12,000, kutoka Km 4,000 tangu kuanzishwa kwake.
Katika hatua nyingine, amebainisha kuwa tangu mwaka 2017, TANROADS ilipopewa jukumu la kujenga viwanja vya ndege, miradi nane imekamilika na miradi tisa ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Kwa ujumla, amesema majukumu ya TANROADS ni pamoja na ujenzi na matengenezo ya barabara, viwanja vya ndege na madaraja, pamoja na usimamizi wa mizani ili kudhibiti magari yenye uzito mkubwa yasiharibu miundombinu ya barabara.