News

WAZIRI KAMWELWE AAGIZA WALIOJENGA JIRANI NA UWANJA WA NDEGE WA NJOMBE WAONDOLEWE

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Njombe na Halmashauri yake pamoja na uongozi wa kiwanja cha ndege cha mkoa huo kuona namna  ya kuziondoa nyumba zote zilizopo mita 500 kutoka katika kiwanja hicho ili kupisha ujenzi unaotarajiwa kufanyika katika kiwanja hicho hivi karibuni.

Waziri Mhandisi Kamwelwe ametoa wito agizo hilo mkoani humo mara baada ya kutembelea kiwanja hicho na kujionea nyumba zilizojengwa kwenye hifadhi ya kiwanja hicho.

Amesema kuwa ujenzi wa makazi hayo umesababishwa na Halmashauri kupima viwanja mpaka kwenye maeneo ya kiwanja hicho hivyo ni lazima waangalie namna sahihi ya kuwahamisha wakazi hao kwa kuwalipa fidia kwa wale wnaaostahili.


“Kiwanja hiki kipo eneo zuri la tambarare, lakini tumeona wenyewe wananchi wamejenga hadi magorofa katika maeneo karibu ya kiwanja hivyo ni lazima waondolewe ili kupisha ukarabati na watakaoonekana wanahaki ya kufidiwa wafidiwe,” amesema Waziri Mhandisi Kamwelwe.


Aidha, Mhandisi Kamwelwe amefafanua kuwa eneo hilo ambalo limejengwa ndio linalotumiwa na ndege kupaa, hivyo kama itashindwa kupaa au kutua inaweza kutua juu ya paa la nyumba ya wakazi hao na kusababisha maafa.

Ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kujenga kiwanja cha ndege cha kimataifa mkoani humo hivyo ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili
kuhakikisha ujenzi huo unaanza.

Waziri Kamwelwe ameeleza kuwa ukamilikaji wa ujenzi wa kiwanja hicho utawezesha usafirishaji wa maua yanayolimwa mkoani humo kwani limekuwa ni tatizo katika usafirishaji kwa kuwa hayawezi kukaa muda mrefu kwenye magari.


Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa na Njombe, Bi. Hana Kibopile, amemshukuru Waziri huyo kwa kutoa agizo hilo kwani limekuja wakati muafaka kwa kuwa wananchi wanauhitaji sana na kiwanja hicho kwani mbali na eneo zuri pia kiwanja hicho kina historia kubwa sana.

Katika hatua nyingine Waziri Kamwelwe amekagua  nyumba ya makazi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe na nyumba ya Katibu Tawala na ujenzi wa ofisi ambayo itakuwa ya Mkoa na kuwataka Wakala wa Majengo (TBA) kuhakikisha majengo ya Serikali yanazingatia ubora na viwango ili kupata thamani ya fedha katika miradi hiyo.