News

SERIKALI YAFUNGA LIFTI 12 KWENYE JENGO LA KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA CHA MSALATO 

SERIKALI YAFUNGA LIFTI 12 KWENYE JENGO LA KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA CHA MSALATO 

Dodoma, 10 Desemba, 2025

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imefunga lifti 12 zitakazotumika na wasafiri watakaopanda ghorofa ya kwanza na pili kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, kilichopo Jijini Dodoma.

Mhandisi anayesimamia ujenzi huo, Mahona Luhende amesema lifti hizo zipo upande wa kuondoka na kuwasili kwa abiria wa Kimataifa na wa ndege za ndani.

Mhandisi Mahona amesema mbali na mfumo huo wa lifti hizo pia wasafiri na wasindikizaji wataweza kutumia ngazi zitakazowafikisha eneo wanalokwenda.

Pia amesema wamefunga eskaleta 22 ambazo zitakuwa zikitumika sambamba na njia nyingine zzitakazotumiwa na wasafiri na wasindikizaji watakaokuwa wakitumia jengo hilo.

Hatahivyo, Mhandisi Mahona amesema ujenzi wa jengo la abiria utekelezaji wake umefikia asilimia 65 baada ya ongezeko la kazi, ambapo pia mkandarasi anaendelea na ujenzi wa majengo ya hali ya hewa, zimamoto na uokoaji, kituo cha kupoozea umeme na jengo la kuongozea ndege.

Pia ujenzi wa miradi ya miundombinu ya barabara ya kutua na kuruka kwa ndege yenye urefu wa Km.3.6 na upana wa mita 60, pia barabara mbili za C na D za kuingia eneo la maegesho zenye urefu wa mita 360 na upana wa mita 44 na maegesho ya ndege yenye urefu wa mita 480 na upana mita 240, halikadhalika barabara za kuingia na kutoka kiwanjani hapo zenye urefu wa Km 5 vyote utekelezaji wake umefikia asilimia 95, ambapo sasa ujenzi upo kwenye hatua ya kuweka alama za kudumu zitakazomwenzesha rubani kutumia vyema barabara hiyo.

 Mhandisi Mahona amesema kazi nyingine za ujenzi zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa eneo la maegesho ya magari takribani 500 kwa wakati mmoja,  uchimbaji wa visima vikubwa na kulaza mfumo wa mabomba yatakayotoa maji ya kutumika kiwanjani hapo kwa muda wote; kujenga uzio wa usalama wenye urefu wa Km. 41 na uchimbaji wa mashimo na mifereji ya kupitishia majitaka.

“Kule nje yaani miundombinu ya barabara, mkandarasi anaendelea na kazi ya kusimika taa za kumwongoza rubani anapopaa na kutua, pia alama kwenye maegesho ya ndege na kwenye madaraja matano ambayo yatatumika na abiria wanapowasili au kuondoka nchini, hususan kwa ndege zinazokwenda nje ya nchi,” amesema Mhandisi Mahona.

Mhandisi Mahona amesema ujenzi wa miradi hiyo inayogharimu kiasi cha  Tshs.Bilioni 165.63 kwa miundombuni ya nje na miundombinu ya majengo ni kiasi cha Tshs. Bil.194.4, ambapo serikali inashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), utamalizika Mei 2026.