MHANDISI KYANDO APEWA HESHIMA KILIMANJARO KWA USIKIVU NA UCHAPAKAZI
Moshi-Kilimanjaro, 29 Novemba, 2025
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando, amepata pongezi kubwa kutoka Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro kutokana na uongozi wake bora, usikivu, na utendaji mzuri katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu hususan barabara mkoani humo.
Akizungumza hivi karibuni na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Nurudin Babu, amesema kuwa Wizara ya Ujenzi ina jukumu nyeti la kuhakikisha wananchi wanapata barabara bora ili kufanikisha usafirishaji wa bidhaa na wananchi ambapo pia amebainisha kuwa Kilimanjaro inashirikiana kwa karibu na TANROADS katika miradi ya barabara.
“Wizara yako ni nyeti sana; ili wananchi wafike kila mahali wanapopataka ni lazima wawe na barabara. Una jukumu kubwa sana lakini umeanza vizuri, na sisi hapa Kilimanjaro hatukumaliza. Tunakudai kwa zile barabara zetu ambazo ujenzi wake umeanza na unaendelea,” alisema Mkuu wa mkoa Mhe. Babu.
Mkuu wa Mkoa pia ameeleza kuwa TANROADS chini ya uongozi wa Mhandisi Kyando inajivunia Meneja ambaye ni msikivu, mwenye weledi wa kazi, na anayehakikisha ushirikiano wa karibu na wadau wote.
“Tunaye Meneja mzuri sana wa TANROADS, Mhandisi Motta Kyando. Anafanya kazi yake vizuri, msikivu, na anapohitajika katika vikao anawasikiliza wote wakiwemo wabunge na kuwapa majibu,” aliongeza.Mkoa wa Kilimanjaro unashirikiana na Meneja Kyando kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo vikao vya Bodi ya Barabara (Road Board), kuhakikisha miradi ya barabara inakamilika kwa ubora na kwa wakati.
Uongozi wa Mhandisi Kyando unaelezwa kuwa ni wa mfano, ukizingatia kutimiza majukumu kwa wakati, kusikiliza changamoto za wananchi na wabunge, na kuhakikisha miradi ya barabara inachangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.