News

WAZIRI ULEGA: TAA ZA BARABARANI DARAJA LA HEDARU KUWEZESHA BIASHARA USIKU NA MCHANA

WAZIRI ULEGA: TAA ZA BARABARANI DARAJA LA HEDARU KUWEZESHA BIASHARA USIKU NA MCHANA

Same-Kilimanjaro, 28 Novemba, 2025,

Habari njema kwa wakazi wa Hedaru! Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, ameeleza kuridhishwa na kasi na ubora wa ujenzi wa Daraja la Hedaru Wilaya ya Same, Kilimanjaro, ambalo sasa limefikia asilimia 95%. Akiwa katika ziara ya kukagua mradi huo, Waziri Ulega alisema kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta matokeo ya kweli kwa wananchi. Alisema, “Serikali inataka kuona miradi kama hii ikibadilisha maisha ya wananchi moja kwa moja.”

Katika ziara hiyo, Waziri Ulega alimuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando, kuhakikisha taa za barabarani zinawekwa katika eneo la daraja ili wakazi wa Hedaru waweze kufanya biashara usiku na mchana. Akitoa maelekezo hayo, Waziri Ulega alisema, “Tunataka Hedaru iwe salama na shughuli ziendelee muda wote. Ufungaji wa taa utawapa wananchi uhuru wa kufanya biashara bila hofu.”

Waziri Ulega pia alimsifu mkandarasi wa kizawa, J.P Traders Ltd, kwa kufanya kazi nzuri. Alisema, “Niwapongeze J.P Traders - ni kampuni ya kizawa inayofanya kazi bora sana. Hii inaonyesha kuwa wakandarasi wetu wa ndani wana uwezo mkubwa.”

Awali, Mhandisi Kyando aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi na kueleza kuwa kazi za mwisho zinaendelea vizuri. Alisema kuwa uwekaji wa lami umekamilika na kwamba mradi upo katika hatua ya kukamilisha mifereji ili kuhakikisha maji yanapita salama bila kuathiri barabara au maeneo ya makazi. Aliongeza kuwa baada ya hapo, mkandarasi ataweka alama za barabarani na miundombinu yote ya usalama kama alivyoagiza Waziri.

Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.495, fedha zinazotolewa na Benki ya Dunia, na unasimamiwa na TANROADS kupitia timu ya TECU Kilimanjaro kwa ushirikiano na Makao Makuu. 

Mara utakapokamilika, daraja hili litaongeza kasi ya biashara, kurahisisha usafiri, kukuza uchumi wa eneo la Hedaru na kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara.