UJENZI DARAJA LA HEDARU WAFIKIA ASILIMIA 95, MENEJA KYANDO AONESHA UONGOZI IMARA, WAZIRI ULEGA AFANYA UKAGUZI
Same-Kilimanjaro, 28 Novemba, 2025
Ujenzi wa Daraja la Hedaru umefikia asilimia 95, huku kazi za mwisho zikikamilishwa ili kuruhusu barabara kupitiwa salama msimu mzima.
Mhandisi Motta Kyando, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro, alitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo moja kwa moja mbele ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, wakati akifanya ukaguzi wa mradi. Kyando ameonyesha usimamizi wa karibu na ufuatiliaji wa kina, hatua inayohakikisha mradi unafanikishwa kwa ubora unaotakiwa.
Daraja hilo litasaidia kupitisha maji kwa ufanisi na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao bila kuathiriwa na mafuriko yanayoharibu miundombinu ya eneo hilo. Mradi unatekelezwa na kampuni ya J.P Traders Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.495, fedha zote zikitolewa na Benki ya Dunia.
“Kazi ya kuweka lami imeshakamilika. Sasa tunaendelea na ujenzi wa mitaro na alama za barabarani ili kuhakikisha usalama kwa watumiaji wote,” alisema Kyando.
Mradi unatarajiwa kukabidhiwa mara kazi za mwisho zikikamilika, huku ukiongeza uchumi na usafiri salama kwa wananchi wa Hedaru na maeneo jirani.