News

TANROADS ARUSHA YAKAMILISHA MATENGENEZO YA BARABARA YA KIKATITI–KINGORI

TANROADS ARUSHA YAKAMILISHA MATENGENEZO YA BARABARA YA KIKATITI–KINGORI

Arusha, 06/11/2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha imekamilisha matengenezo ya kilomita moja na nusu ya barabara katika eneo la Kikatiti–Kingori, katika barabara kuu inayounganisha mikoa ya Kilimanjaro na Tanga na kuingia Jiji la Arusha.

Akizungumza jijini Arusha, Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo Mkoa wa Arusha, Mhandisi Christopher Saul, amesema kuwa matengenezo hayo yamefanyika baada ya barabara hiyo kuchakaa kutokana na muda mrefu wa matumizi, tangu ilipojengwa mwaka 1996.

“Tuliona ni muhimu kufanya matengenezo katika eneo hili kutokana na nafasi kubwa ya barabara hii kiuchumi. Hii ni njia kuu ya kuingia Arusha kutoka Kilimanjaro na Tanga, hivyo ilikuwa na uhitaji mkubwa wa matengenezo,” alisema Mhandisi Saul.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa kazi hiyo ulifanyika kufuatia maelekezo ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, aliyetoa agizo la kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyoharibika ili kuwezesha shughuli za usafirishaji kuendelea bila usumbufu.

Mhandisi Saul ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kulinda miundombinu iliyopo, akisisitiza kuwa serikali hutumia fedha nyingi katika ujenzi na matengenezo ya barabara.

“Tunawaomba madereva wawe makini kwa kutozidisha mizigo katika magari yao, kwani kufanya hivyo huharibu barabara. Pia ni muhimu kulinda alama za barabarani kwa kuwa zinaongoza madereva na kusaidia kuepusha ajali,” alisisitiza.

Aidha, amekemea vitendo vya baadhi ya wananchi kuiba vifaa vya barabara kama chuma chakavu, akisema kitendo hicho kinailetea hasara serikali na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Akizungumzia mchango wa barabara hiyo katika maendeleo ya kiuchumi, Mhandisi Saul amesema kuwa njia hiyo ni muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa na abiria, hususan watalii wanaowasili kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuelekea mbuga za wanyama na vivutio vya utalii kama Mlima Kilimanjaro na pia inarahisisha biashara na usafiri kati ya mikoa ya jirani na nchi ya Kenya.

Mwisho, Mhandisi Saul ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha kukamilika kwa matengenezo hayo, akisema hatua hiyo imeendelea kuboresha usafiri na kukuza uchumi wa mkoa wa Arusha na taifa kwa ujumla.