News

MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA YABADILISHA TABORA KIMIUNDOMBINU YA BARABARA, MADARAJA NA VIWANJA VYA NDEGE

MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA YABADILISHA TABORA KIMIUNDOMBINU YA BARABARA, MADARAJA NA VIWANJA VYA NDEGE

Tabora

29 Septemba, 2025

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Tabora umeendelea kushughudia mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kupitia miradi mikubwa ya ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na uwanja wa ndege, hatua ambayo imeufungua mkoa huo na kuuweka kwenye ramani ya Kitaifa na Kikanda kwa maendeleo ya miundombinu.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji, amesema Tabora ndio mkoa mkubwa zaidi nchini kwa mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 2,188.06, kati ya hizo, kilomita 1,077.12 ni Barabara Kuu, huku kilomita 1,073.37 ni barabara za mkoa na kilomita 37.6 ambazo zimegawanyika katika kiwango cha lami na changarawe huku barabara ya Igunga–Mbutu–Igulubi (sehemu ya Mwagala) yenye jumla ya kilomita 37.6 ikiwa imekasimiwa TANROADS.

 “Kwa ujumla, changamoto bado zipo, lakini mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka minne ya Rais Samia ni makubwa na yanaonekana kwa macho, kwa ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji” anasema Mhandisi Mlimaji.

Amesema hadi sasa TANROADS Tabora imefanikisha miradi mikubwa saba iliyokamilika, ikiwemo madaraja matatu na zaidi ya kilomita 500 za barabara za lami zilizojengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 489.Miongoni mwa madaraja hayo ni Kizenge na Nyahua katika barabara ya Manyoni–Tabora pamoja na daraja kubwa la Koga lenye urefu wa mita 120 katika barabara ya Tabora–Mpanda, ambapo ni hatua kubwa inayorahisisha usafiri na usafirishaji katika ukanda wa kati wa Tanzania.

Aidha, miradi mingine saba inaendelea kutekelezwa, ikiwemo usanifu wa barabara ya Kuso (Km 69), Ziba–Choma (Km 109), Tabora–Ulyankulu, na barabara za kuzunguka mji (bypass) zenye jumla ya kilomita 90. Katika barabara ya Ziba–Choma, usanifu umefikia zaidi ya asilimia 90 na tayari kilomita 11 zimetangazwa zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Tabora umefikia asilimia 97 huku kazi zilizobaki zikiwa ni ufungaji wa jenereta na mifumo ya mizigo, na inatarajiwa kufikia mwezi Oktoba 2025 kiwanja hicho kitakamilika kwa asilimia 100.

Mradi wa Kiwanja cha ndege cha Tabora una thamani ya Shilingi milioni 488 na unahusisha pia ujenzi wa uzio wa usalama yenye urefu wa kilomita 6.25, maegesho ya magari 54 na barabara ya kuingilia yenye urefu wa mita 375.

Kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja, jambo linalotarajiwa kuongeza idadi ya watalii na wafanyabiashara wanaotumia mkoa wa Tabora kama kitovu cha safari zao.

Mbali na miradi hiyo, serikali pia imetoa kipaumbele kwa barabara ya Ipole–Rungwa yenye urefu wa kilomita 172.4, ambayo usanifu wake ulimalizika mwaka 2020 ambapo pia tayari daraja la Msuva lenye urefu wa mita 10 limekamilika kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.65.

Kwa upande wa bajeti, Mhandisi Mlimaji amesema kila mwaka mkoa hutumia wastani wa Shilingi Bilioni 22 kwa matengenezo ya kawaida ya barabara na kati ya Shilingi Bilioni 4 hadi 8 kwa miradi ya maendeleo, na hadi sasa zaidi ya Shilingi Bilioni 150 zimetumika kwa ukarabati na matengenezo, yakihusisha zaidi ya wakandarasi 10 wazawa.

Katika utekelezaji wa sera ya serikali ya kutoa asilimia 30 ya zabuni kwa makundi maalumu, mkoa wa Tabora umeajiri wakandarasi wanawake saba katika mwaka wa fedha 2024/2025 na zaidi ya asilimia 90 ya ajira kwenye miradi hii yote imetolewa kwa wakandarasi wazawa.

Kwa wakulima na wafanyabiashara, barabara bora zinamaanisha bidhaa na mazao kufika sokoni kwa wakati, huku sekta ya utalii ikitarajiwa kunufaika zaidi kupitia kiwanja cha ndege mpya, aidha, wananchi wametakiwa kuheshimu hifadhi za barabara na kufuata sheria ili kulinda thamani ya miundombinu.

Meneja huyo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za miradi hiyo,  pia amewapongeza Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Mhandisi Aisha Amour na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta kwa ushirikiano wao wa karibu.