WAHANDISI WAHIMIZWA KUFANYA MAZOEZI KUJIEPUSHA NA MAGONJWA
Dar es Salaam28 Septemba, 2026
Wahandisi wamehimizwa kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujiepusha na magonjwa nyemelezi, yatakayowakwamisha kuendelea na kazi zao.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni wakati wa mbio za marathoni za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Mhandisi George Daffa, Meneja wa Kitengo cha Usalama Barabarani wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), ambaye alishiriki mbio hizo zilizoanzia Chuo Kikuu cha Dar es Salaama kwa kukimbia kilometa 10.
Mha. Daffa amesema kufanya mazoezi ya mara kwa mara kunaongeza ufanisi wa kazi, na kujiepusha na magonjwa ya moyo na kisukari.
“Tufanye mazoezi maana tunajenga afya zetu, kwani tunapofanya kazi mazoezi ni lazima, ili afya zisitetereke kwa kupata magonjwa ya presha kwani jioni mtu unaweza kukimbia kilometa tano au saba ili kujiweka sawa,” amesema Mha. Daffa.
Naye Joyce Francis, Mtaalam wa Mambo ya Kijamii wa TANROADS amewashauri watumishi wenzake kufanya mazoezi kwa bidii ili kuzilinda afya zao.
“Mimi nimekimbia kilometa 10 kwenye hii ERB Marathon nawashauri wenzangu kutenga muda kwa ajili ya mazoezi hata mara mbili kwa wiki wakimbie kilometa mbili, tano na kuendelea,” amesisitiza Joyce.