MKUTANO WA 22 WA WAHANDISI NI DIRA YA KAZI ZAO – MHANDISI MALULI WA TANROADS
Dar es Salaam, 26 Septemba 2025
Mkutano wa 22 wa mwaka wa wahandisi nchini, uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 25–26 Septemba 2025, umeelezwa kuwa kielelezo cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mhandisi Emmanuel Maluli kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) alisema kuwa mkutano huo uliwakutanisha washiriki wa ndani na nje ya nchi, ambapo mijadala muhimu iliangazia namna ya kutekeleza majukumu ya ujenzi katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Kwa mujibu wa Mhandisi Maluli, Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 imetekelezwa kwa kiasi kikubwa, jambo lililowezekana kutokana na serikali kutenga fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya maendeleo, ambayo sasa ni chachu ya kukuza uchumi na pato la taifa.
Mhandisi Maluli alisema mkutano huo ambao umefunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, na kufungwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, umekuwa wa mafanikio makubwa. Washiriki wote—waliokuwapo ukumbini na wale waliounganishwa kwa njia ya mtandao—wamenufaika. Jambo kubwa alilojifunza ni umuhimu wa wahandisi kusajiliwa kwenye Bodi ya Usajili na kula kiapo kinachowataka kuwajibika kwa uadilifu na uaminifu katika kusimamia miradi ya maendeleo, ili kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, alisisitiza kuwa wahandisi ndio uti wa mgongo wa utekelezaji wa miradi ya sekta mbalimbali, na iwapo watazembea au kutofuata miiko na taaluma, miradi inaweza kukosa viwango vinavyohitajika na kusababisha hasara kubwa kwa taifa. Kwa mantiki hiyo, aliwataka wahandisi kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora na kudumu kulingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na serikali.
Mhandisi Maluli pia alibainisha kuwa, kwa upande wa TANROADS, uhakiki wa ubora wa miradi yote hufanywa kupitia kitengo cha maabara na utafiti, jambo linalosaidia kudhibiti viwango vya kazi zinazotekelezwa.
Aliongeza kuwa mwaka huu mkutano wa ERB umefanikiwa sana. Ameshiriki zaidi ya mikutano kumi na viongozi wameweza kuwapa motisha kubwa. Pia, wahandisi wapya wameendelea kuapa na kusajiliwa kupitia mifumo ya kisasa, jambo linaloonyesha kuwa mwelekeo wa taaluma hiyo ni mzuri zaidi.
Kwa upande wake, Mhandisi Emmanuel Tang’are alisema wanajivunia kushiriki katika mkutano huo wa 22 wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kwani umekuwa jukwaa la kujifunza kutoka kwa wengine. Alishauri wahandisi wengi zaidi washiriki kwenye mikutano ya kitaaluma kwa kuwa inapanua upeo, kuongeza maarifa na kutoa mbinu za kutatua changamoto wanazokutana nazo kwenye majukumu yao ya kila siku.
Aliongeza kuwa wanashukuru serikali kwa kuanzisha taasisi hii inayoshughulikia wahandisi, kwa kuwa imefanikisha maandalizi ya mikutano yenye tija kubwa. Aidha, mikutano hiyo inasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wahandisi na hata wakandarasi.
Wakati akifunga mkutano huo, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, aliitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuwachukulia hatua za kinidhamu wahandisi watakaokiuka sheria na taratibu za taaluma, ikiwemo kutopangiwa kazi nyingine wale watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kutofuata miiko ya taaluma.
Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa:“Wajibu wa Wahandisi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”