News

TANROADS YAWAALIKA WAHANDISI KUWEKEZA MSALATO AIRPORT

TANROADS YAWAALIKA WAHANDISI KUWEKEZA MSALATO AIRPORT

Dar es Salaam, 26 Septemba 2025

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imewaalika wahandisi kushiriki na kuwekeza katika fursa mbalimbali zilizopo kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato, kinachojengwa jijini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa na Mhandisi Donatus Benamungu wa TANROADS wakati akiwasilisha mada kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa na taasisi hiyo katika Mkutano wa 22 wa Wahandisi Nchini, unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Benamungu amesema kuwa jengo la abiria la Msalato litaweza kuhudumia ndege 16 za kimataifa kwa wakati mmoja, ambapo kati ya hizo, ndege tano zitakuwa na nafasi ya kuegeshwa kwenye madaraja ya kuingilia moja kwa moja. Aidha, kiwanja hicho kitakuwa na eneo kubwa la kuegesha magari pamoja na nafasi pana kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli mbalimbali.

“Hiki kiwanja kina jengo kubwa la abiria, na kinabarabara ya kuruka na kutua ndege yenye urefu wa kilomita 3.6, ambayo ni ya tatu kwa urefu nchini baada ya viwanja vya ndege vya Mwanza na KIA,” alisema.

Kwa mujibu wa Mhandisi Benamungu, usalama wa kiwanja hicho pia umezingatiwa, ambapo kutajengwa uzio maalumu ili kuimarisha ulinzi na kuzuia wahalifu wanaoweza kuhatarisha usalama wa mali na abiria watakaolitumia.

Ameongeza kuwa mbali na mradi huo wa Msalato, TANROADS pia inatekeleza miradi mingine mikubwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko jijini Dodoma yenye lengo la kupunguza msongamano wa magari, sambamba na ujenzi wa daraja la Pangani.