TANROADS YAWAALIKA WAHANDISI KUWEKEZA MSALATO AIRPORT
Dar es Salaam
26 Septembaa, 2025
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imewaalika wahandisi kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato kinachojengwa jijini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa na Mhandisi Donatus Benamungu wa TANROADS wakati akiwasilisha mada ya miradi ya kimkakati inayofanywa na taasisi hiyo, kwenye Mkutano wa 22 wa mwaka wa wahandisi nchini, unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Mha. Benamungu amesema jengo la Msalato litaweza kuhudumia ndege 16 za Kimataifa kwa wakati mmoja, na kati ya hizo ndege tano zitaweza kuegeshwa kwenye madaraja, pia kiwanja hicho kinaeneo kubwa la kuegesha magari na inaeneo kubwa kwa ajili ya kuwekeza shughuli mbalimbali.
“Hiki kiwanja kina jengo kubwa la abiria, na linabarabara ya kutua na kuruka ndege yenye Km. 3.6, ambayo ni ya tatu kwa urefu baada ya zile za viwanja vya ndege vya Mwanza na KIA,” amesema Mha. Benamungu.
Halikadhalika, amesema kiwanja hicho kitakuwa na usalama wa kutosha kwa kuwa kutajengwa uzio wa usalama, ili kuzuia wahalifu wanaoweza kuhatarisha usalama wa mali pamoja na abiria watakaokuwa wakitumia kiwanja hicho.
Mha. Benamungu amesema mbali na mradi huo wa Msalato pia TANROADS inajenga barabara ya mzunguko jijini Dodoma, ambayo ni mahususi kwa kupunguza foleni, na pia wanajenga daraja la Pangani.
MWISHO