TANROADS MWANZA YAWAALIKA WANANCHI KUPIMA MALIGHAFI ZA UJENZI ILI KUKIDHI VIWANGO
Mwanza, 24 Septemba 2025
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza imewaalika wajenzi wa miradi mbalimbali, ikiwemo ya miundombinu ya barabara na nyumba za makazi, katika Jiji la Mwanza na mikoa jirani, kutumia maabara yake ya kisasa kwa ajili ya kupima malighafi za ujenzi. Hatua hii inalenga kuhakikisha viwango vinazingatiwa na kujenga makazi bora yatakayodumu kwa muda mrefu.
Meneja wa TANROADS Mwanza, Mhandisi Pascal Ambrose, amesema hivi karibuni kuwa maabara hiyo, ambayo imesajiliwa kisheria, inatoa huduma za upimaji kwa gharama nafuu.
Mhandisi Ambrose alibainisha kuwa maabara hiyo imebeba vifaa vya kisasa vinavyoweza kupima ubora wa mchanga, kokoto, lami, udongo, maji, zege, matofali na malighafi nyingine za ujenzi.
Mhandisi Ambrose alisema, “Tunawashauri watu waje kupima malighafi zao kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali. Maabara yetu imesajiliwa, ina vifaa vya kisasa kabisa na itawasaidia kuhakikisha ujenzi wao unakidhi viwango na kudumu kwa muda mrefu.”
Kwa upande wake, mtaalam wa maabara hiyo, Kalokola Ruzibukya, alisema maabara hiyo ina wataalam wa kutosha na hufuata mifumo rasmi ya ukaguzi ili kutoa majibu sahihi kwa kila sampuli inayopimwa.
Ruzibukya alisema, “Kwa kawaida mtu anapopeleka malighafi, tunafanya uchunguzi na kutoa majibu sahihi kuhusu ubora wa udongo, zege na malighafi nyingine. Ikumbukwe kuwa sisi hatuendi nao wanapojenga; hivyo wakibadilisha na kutumia tofauti na majibu yetu, ujenzi hauwezi kuwa sahihi. Kujenga kiholela bila kujua uwezo wa vifaa ni hatari.”
Ameeleza kuwa, kwa mfano, katika upimaji wa kokoto hutumia mashine yenye mizunguko 500, kisha kuzigawanya kwenye vichekecheo vya ujazo mbalimbali, ili kubaini kiwango cha kokoto kilichovunjika na kutoa majibu sahihi ya ubora wake.
Naye Mathias Alfred kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Buchosha, alisema wao wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya majengo na wameona umuhimu wa kutumia maabara hiyo ili kuhakikisha uimara wa majengo.
Bw. Alfred alisema, “Nashauri wajenzi wengine kuhakikisha malighafi wanazotumia zinapimwa katika maabara ya TANROADS ili kupata ushauri wa kitaalam, hatua ambayo itasaidia kujenga majengo bora, imara na yanayodumu kwa muda mrefu.”