News

TANROADS MWANZA YATAHADHARISHA UWIZI WA ALAMA ZA BARABARANI

TANROADS MWANZA YATAHADHARISHA UWIZI WA ALAMA ZA BARABARANI

Mwanza, 23 Septemba 2025

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza umewatahadharisha baadhi ya wakazi wasio waaminifu wa jiji hilo kuacha mara moja vitendo vya wizi wa miundombinu ya alama za barabarani, kwani alama hizo zina umuhimu mkubwa kwa madereva katika kutambua mazingira ya barabara wanazopita.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Pascal Ambrose, amesema alama za barabarani zinamsaidia dereva, awe ni mgeni au mwenyeji, kuelewa mazingira ya eneo analopita. Ametoa mfano kuwa pale panapowekwa alama ya wanafunzi kuvuka au alama ya tuta, dereva anatakiwa kupunguza mwendo kwa ajili ya usalama.

Mhandisi Ambrose amesema kuibiwa kwa alama hizo husababisha madhara makubwa kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara, kwani mara nyingi hupelekea ajali kwa kutokuwepo taarifa sahihi kuhusu kinachoendelea mbele. Ametoa ufafanuzi kwamba dereva anaweza kutojua kama barabara ni nyembamba au kuna daraja endapo alama zimeondolewa.

“Dereva kama ni mgeni, na hata kama sio mgeni, alama zinamsaidia mahususi kutambua mbele kunakuwa na nini. Na kama zimeng’olewa na kuibwa, basi anaweza asitambue lolote lililopo mbele yake na badala yake akajikuta akipata ajali,” amesema Mhandisi Ambrose.

Aidha, amewataka viongozi na wananchi kushirikiana kwa kutoa taarifa kuhusu wale wanaohujumu miundombinu hiyo ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.

Imedaiwa kuwa alama hizi huibwa kisha hubadilishwa na kuuzwa kama vyuma chakavu, ambapo biashara hiyo imeonekana kushamiri zaidi katika maeneo ya kata za Mabatini, Igoma na Buhongwa.