MTENDAJI MKUU TANROADS AFANYA UKAGUZI WA KUSHTUKIZA MRADI WA BRT UBUNGO–KIMARA, ATOA MAAGIZO YA UKAMILISHAJI
Dar es salaam
19/9/2025
Dar es Salaam, Septemba 19, 2025 – Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, leo amefanya ukaguzi wa kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Kwanza, Package A, kutoka Ubungo hadi Kimara, na kutoa maelekezo ya kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Mradi huu wenye thamani ya shilingi bilioni 83.8 unafadhiliwa na Benki ya Dunia, na hadi sasa umefikia takribani asilimia 60 ya utekelezaji. Hii ni hatua kubwa ikilinganishwa na miezi tisa iliyopita ambapo mradi ulikuwa umefikia asilimia 21 pekee.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mhandisi Besta alisema upanuzi wa barabara kutoka njia nne hadi sita ni hatua muhimu itakayosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari.
"Miradi yote ya BRT kuanzia Awamu ya Kwanza hadi ya Nne (Lot 1 na 2) inaendelea jijini Dar es Salaam, na TANROADS itaendelea kusimamia ubora wa ujenzi ili kupunguza msongamano wa magari," alisema.
Aidha, aliwataka wakandarasi kuongeza kasi ya kazi kutokana na mvua zinazotarajiwa kuanza, akisisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi mapema ili wananchi wapate nafuu ya usafiri.
"Ni lazima tuongeze nguvu ili mradi ukamilike kwa wakati na kutoa nafuu ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam," alisisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa BRT, Mhandisi Allen Natai, alisema mkandarasi anaendelea na kazi na amepewa ushauri wa kuendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, alisema wamepokea maelekezo ya Mtendaji Mkuu na watahakikisha wanayatekeleza kwa vitendo, huku wakimsukuma mkandarasi kukamilisha kazi kabla ya msimu wa mvua kuanza.