News

UJENZI WA MADARAJA SABA ENEO LA KILEO KUIFANYA BARABARA YA ARUSHA-MOSHI KUPITIKA WAKATI WOTE

UJENZI WA MADARAJA SABA ENEO LA KILEO KUIFANYA BARABARA YA ARUSHA-MOSHI KUPITIKA WAKATI WOTE

Kilimanjaro

01 Sept, 2025

Kaimu Meneja mkoa wa Kilimanjaro mhandisi Benitho Mdzovela wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa madaraja saba katika eneo la Kileo ambao ni mradi wa pili katika miradi inayotekelezwa mkoani humo kwa maeneo yaliyoathiriwa na mvua za el-nino zilizonyesha novemba 2023 hadi mei 2024.

Aidha mhandisi Mdzovela ameeleza kuwa kipindi cha mvua eneo hilo lilisababisha barabara kutopitikia kwa masaa kadhaa kutokana na maji kupita juu ya barabara na kuzuia shughuli za kiuchumi katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha na nchi jirani ya Kenya, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutaleta tija kwa watumiaji barabara hiyo na wananchi wote kwa ujumla.

"Katika eneo hili tunajenga madaraja saba ambayo yana ukubwa wa mita tano kwa maana ya upana wake na kimo cha mita mbili na nusu, pia tunainua tuta kwa kipande hiki kwa kimo cha mita moja na nusu na uinuaji wa tuta hili unafanyika kwenye kipande chenye urefu wa mita elfu moja na mia sita" Amesema mhandisi Mdzovela

"Mradi huu unatekelezwa na kusimamiwa TANROADS kupitia kitengo cha TECU mkoa wa Kilimanjaro na unafadhiliwa na Benki ya Dunia."Mradi huu ulisainiwa tarehe 10/2/2025 na mradi unatarajiwa kukamilika tarehe 21/12/2025 na gharama za utekelezaji wa mradi huu ni shilingi Bilioni 6.8, utekelezaji wa mradi huu unahusisha ujenzi wa madaraja saba na unyanyuaji wa tuta la barabara kwa kipande cha urefu mita 1600" Amesema mhandisi Mdzovela

Upana wa barabara utakuwa mita saba na nusu na mabega ya barabara mita mbili kila upande, utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 31 kama mnavyoona madaraja yote yamekwisha kujengwa na kukamilika kinachoendelea sasa ni kazi ya kuinua tuta.Mradi huu umekuwa na manufaa kwa wananchi kwani umezalisha ajira zipatazo 67 ambapo jumla ya wanawake 12 na wanaume 55 wameajiriwa kusaidia ujenzi wa mradi huo.

Mpaka leo mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali kiasi cha shilingi Bilioni mbili na  elfu sitini lakini pia amewasilisha hati ya malipo kwa kazi ambazo zimekwisha fanyika yenye thamani ya bilioni moja na milioni mia saba arobaini na tisa na taratibu za malipo zinaendelea kufanyiwa kazi ni imani yetu mkandarasi atalipwa baada ya siku chache zijazo.

”Nichukue nafasi hii kuwasihii watumiaji wa barabara ambao wanatumia barabara ya pembeni ya mchepuko tunajua ya kwamba hali yake haiwezi kuwa nzuri sana ukilinganisha na pale mradi huu utakuwa umekamilika kuwa watuvumilie kwenye kipindi hiki tunatekeleza mradi huu kwa kuhakikisha tunafanya kazi usiku na mchana ili mradi huu ukamilike kwa wakati” amesema.

Halikadhalika, Kaimu Meneja ameishukuru serikali ya Tanzania inayoongozwa mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo waliweza kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu.

Naye Paul Mwanahima ambaye ni msimamizi  wa mradi kwa upande wa mkandarasi King's Builders ameishukuru serikali kwa kuwajali wazawa kwa kuwapa kazi na kuahidi kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi kwa wakati.