MRADI WA KALVATI RUVU WAKAMILIKA, SULUHU YA KUDUMU YA CHANGAMOTO YA MAFURIKO
Pwani
02 Sept, 2025
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage, amethibitisha kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kalvati katika eneo la Ruvu, kwenye kipande cha barabara kinachounganisha Ruvu Darajani na Vigwaza. Hatua hiyo imeweka historia mpya kwa kuondoa changamoto ya eneo hilo kujaa maji wakati wa mvua za masika.
Mradi huo ulianza tarehe 5 Novemba 2024 na ulikuwa umepangwa kukamilika ndani ya miezi 10. Ulifanikiwa kukamilika kwa wakati na kukabidhiwa rasmi tarehe 1 Septemba 2025.
Kalvati hiyo, yenye midomo minne, imejengwa kwa viwango vya juu vya ubora sambamba na ujenzi wa njia za maingiliano zenye urefu wa mita 480 zilizowekwa lami.
Mafanikio ya mradi huu ni pamoja na kuondoa changamoto ya kuvurugika kwa usafiri na usafirishaji katika eneo la Ruvu, hususan msimu wa mvua, ambapo maji yalikuwa yakijaa barabarani. Changamoto hiyo sasa imepatiwa suluhu ya kudumu na haitarajiwi tena kujitokeza kwa majira yote ya mwaka.
Aidha, michepuo iliyotumika kama njia mbadala wakati wa ujenzi itawekewa alama maalum kuonyesha kuwa siyo njia rasmi.
Mhandisi Mwambage pia ametoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha kwa tahadhari, kutokana na wingi wa magari yanayotumia barabara hiyo. Inakadiriwa wastani wa magari 19,000 hupita kila siku, sawa na magari 740 kwa saa.
Katika hatua nyingine, ameishukuru Serikali kwa kufanikisha mradi huo kupitia upatikanaji wa fedha na kupongeza jitihada zake za kuondoa kero zilizokuwa zikisumbua wakazi wa eneo hilo, pia na wasafiri na wasafirishaji.