Wakazi wa Mabatini Wapongeza Serikali: Kero ya Mafuriko Sasa Historia
Mwanza
31 Agosti, 2025
Shangwe na faraja zimeenea katika mitaa ya Mabatini jijini Mwanza baada ya serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufanikisha ujenzi wa daraja jipya la Mabatini, suluhisho la kudumu kwa kero ya mafuriko yaliyokuwa yakiwakumba wakazi kwa miaka mingi.
Kwa muda mrefu, mvua za masika zilipokuwa zikishuka, wananchi wa eneo hilo walijikuta wakipoteza mali, maisha, na miundombinu kutokana na mafuriko yaliyokuwa yakisomba kila kitu kilichokuwa mbele yake. Lakini sasa, matumaini mapya yameibuka kupitia daraja jipya linalotarajiwa kuwa ngao dhidi ya maafa hayo.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Soko la Mabatini, Bw. Rajabu, mkazi wa eneo hilo tangu 1988, alisema:
“Daraja la zamani lilikuwa hatari hasa wakati wa mvua, na kumbukumbu mbaya zaidi ni mwaka 2000 tuliposhuhudia mafuriko makubwa yaliyosababisha barabara kufungwa kwa muda. Leo hii, tunashukuru serikali kwa daraja hili jipya ambalo litaepusha ajali na kulinda maisha ya jamii.”
Bi. Regina Tumaini, mkazi wa mtaa wa Nyerere B, aliibua hisia kali akisema:
“Nimewahi kupoteza mali na kushuhudia vijana, wanafunzi na waendesha bodaboda wakisombwa na maji. Leo ninashukuru serikali na wataalam kwa mradi huu ambao ninaamini kwa asilimia 100 utamaliza kabisa shida ya mafuriko.”
Kwa upande wake, Bw. Kusekwa Majabu alisisitiza kuwa daraja jipya litaboresha usalama na biashara:
“Awali maji yalikuwa yanapita juu ya daraja na kuondoa uhai wa vijana na wazee. Sasa tunashuhudia historia mpya—eneo letu linakuwa salama na barabara hii ni kiunganishi muhimu kwa magari ya ndani na hata yale ya nchi jirani.”
Akifafanua kuhusu ujenzi, Mhandisi Godfrey Wandi wa kampuni ya Nyanza Road Works alisema mradi huo umefikia asilimia 74 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo 15 Novemba 2025.
“Daraja jipya lina urefu wa mita 26 na limejengwa kwa upana zaidi likiwa na vyumba sita vikubwa vya kupitisha maji kwa wakati mmoja. Aidha, mradi unajumuisha pia ujenzi wa barabara mbili zenye jumla ya urefu wa mita 590 ambazo tayari zipo katika hatua nzuri za ukamilishaji,” alisema Mhandisi Wandi.
Ameongeza kuwa mradi huo umetoa ajira kwa zaidi ya 77 kutoka Mabatini na maeneo jirani, huku wananchi wakinufaika kupitia ajira za moja kwa moja na fursa za biashara ndogo ndogo.
Bi. Winfrida Francis, mmoja wa wananchi waliopata ajira kupitia mradi huo, alisema:“Kwa kweli huu mradi umenisaidia kuongeza kipato changu. Sasa naweza kuendesha familia yangu na hata kuanzisha biashara ndogo ndogo kwa msaada wa kipato ninachopata.”
Daraja la Mabatini linatazamwa kama alama ya matumaini mapya na mabadiliko kwa wakazi wa Mwanza. Kero ya mafuriko iliyodumu kwa miongo kadhaa sasa inaonekana kuelekea ukingoni, huku wakazi wakipongeza serikali kwa kuwekeza kwenye mradi unaolinda maisha, mali na kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi.