SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA BARABARA NA MADARAJA MKOA WA LINDI
Lindi
20 agosti, 2025
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua kubwa za El-Nino, ambapo hadi sasa, jumla ya miradi 13 ya dharura inatekelezwa katika Mkoa wa Lindi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za usafiri wa uhakika na salama. Miradi hiyo inasimamiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi, ambapo akizungumza kuhusu utekelezaji wake, Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Fred Sanga, alisema ujenzi wa madaraja ya Somanga–Mtama, Kipwata na Mkereng’ende umekamilika kwa zaidi ya asilimia 80.
Mha. Sanga amefafanua kuwa mihimili ya madaraja yote tayari imekamilika na baadhi yanasubiri kusimikwa ‘vigirder’ vikubwa (bolti) kwa ajili ya hatua ya mwisho ya ukamilishaji.
Aidha, alieleza kuwa ujenzi wa barabara ya Tingi–Kipatimu unaendelea ambapo kutajengwa makalvati sita na kati yake matatu tayari yamekamilika na mengine yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi, mradi huo unatekelezwa na kampuni ya ME & Co. Ltd, na kazi zinaendelea kwa kasi ili kuhakikisha wananchi hawapati athari za kukosa usafiri.
Akizungumzia umuhimu wa miradi hiyo, Mha. Sanga alisema barabara ya Nangurukuru–Liwale, yenye miradi mitatu ya madaraja, itarahisisha usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara yakiwemo machungwa, ufuta na korosho, na pia litaondoa changamoto zilizokuwa awali katika maeneo ya Miguruwe na Zinga.
Kwa upande wake, Levi Msafiri, mkandarasi kutoka ME & Co. Ltd, alibainisha kuwa serikali imeendelea kutoa fedha kwa wakati na wameahidi kutekeleza miradi hiuo kwa viwango bora vinavyotakiwa.
Hata hivyo, mkandarasi ameendelea kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi hawapati changamoto ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Wananchi pia wametoa shukrani kwa Serikali na mkandarasi kwa jitihada hizo, ambapo Bw. Rashid Said, mkazi wa Lindi amesema sasa wanauhakika wa safari kwa nyakati zote kutokana na sasa hakutakuwa na adha ya mafuriko tena, ambapo yaliyotokea hivi karibuni hayajawahi kutokea tangu mwaka 1985.