WAFANYAKAZI WA TANROADS SONGWE WAKUMBUSHWA KUIMARISHA MAADILI NA UADILIFU
Songwe
15 Agosti, 2025
Kikao cha wafanyakazi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe kilifanyika tarehe 15 Agosti 2025 kikiwa na lengo la kuimarisha maadili, uadilifu na ustawi wa watumishi.
Kikao hicho kiliongozwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, kilienda sambamba na mafunzo ya maadili na uadilifu, katika hotuba yake, aliwakumbusha watumishi umuhimu wa kuzingatia mada zitakazowasilishwa na akasisitiza kuwa elimu hiyo ni nyenzo ya kuongeza ufanisi na mshikamano kazini.
Pia kikao hicho kilihudhuriwa na Afisa Rasilimali Watu wa Kanda, Bw. Edgar Msigala, pamoja na wageni maalum kutoka taasisi mbalimbali.
Kutoka taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), mgeni alitoa mada kuhusu rushwa na uadilifu mahali pa kazi, akisisitiza wajibu wa kila mtumishi kudumisha uwajibikaji na kuepuka vitendo vya rushwa.
Naye Daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Songwe alitoa elimu kuhusu ugonjwa wa UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza, akihimiza wafanyakazi kuzingatia afya bora na mtindo sahihi wa maisha.
Bw. Msigala, Afisa Rasilimali Watu wa Kanda, aliwasilisha mada juu ya maadili katika utumishi wa umma, akisisitiza nidhamu, utii wa sheria na uadilifu kama nguzo kuu za ufanisi wa kazi serikalini.
Mha. Bishanga wakati wa kufunga kikao hicho alisisitiza mada zilizotolewa na kuwataka watumishi kuzitumia katika majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya taifa na taasisi kwa ujumla.