News

TAA KUMULIKA DARAJA LA SIMIYU USIKU NA MCHANA

TAA KUMULIKA DARAJA LA SIMIYU USIKU NA MCHANA

Simiyu

15 Agosti, 2025

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imethibitisha kuwa ujenzi wa Daraja la Simiyu mkoani Mwanza utahusisha uwekaji wa taa maalum, ili kuruhusu daraja kutumika kwa ufanisi wakati wa usiku na mchana. Hatua hii inalenga kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mhandisi wa Madaraja kutoka TANROADS, Edward Nyamhanga, alisema kwa sasa kazi inayoendelea ni ujenzi wa nguzo mlalo, ambapo jumla ya nguzo 13 kati ya 30 zinazohitajika tayari zimekamilika.

"Kwa sasa tupo kwenye maandalizi ya nguzo za mlalo. Zikishakamil8ka tutaanza kuzipanga  darajani kisha kumaliza sehemu ya juu ya daraja,” alisema Mhandisi Nyamhanga.

Daraja hilo litakuwa na upana wa mita 12.3, likiwa na njia za magari na sehemu maalum kwa watembea kwa miguu. Hii itarahisisha magari kupishana kwa usalama, tofauti na daraja la awali lililokuwa jembamba na kuruhusu gari moja pekee kupita kwa wakati mmoja, hali iliyosababisha foleni na usumbufu kwa watumiaji wa barabara.