News

WAKANDARASI WANAWAKE WAZAWA WAKABIDHIWA UJENZI WA BARABARA SONGWE

WAKANDARASI WANAWAKE WAZAWA WAKABIDHIWA UJENZI WA BARABARA SONGWE

Songwe, 14 Agosti 2025

Wanawake wanne, ambao ni makandarasi wazawa, wamekabidhiwa rasmi jukumu la kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 20, itakayounganisha Wilaya za Mbozi na Ileje, mkoani Songwe. Mradi huo utagharimu shilingi bilioni 42.

Makabidhiano hayo yalifanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bw. Jabiri Makame, na kusimamiwa na Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoani humo, Mhandisi Suleiman Bishanga. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha sekta ya ujenzi inawawezesha makandarasi wazawa, hususan makundi maalum kama wanawake.

Mhandisi Bishanga alisema utekelezaji wa mradi huu umewezekana baada ya Rais Samia kufanya marekebisho ya Sheria ya Manunuzi, yaliyolenga kutoa nafasi kwa makundi maalum. Aidha, alibainisha kuwa barabara hii ni sehemu ya miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa mkoani Songwe, ambapo tayari miradi miwili -  barabara ya Mpemba -Isongole na daraja la Kamsamba lenye urefu wa mita 84 katika barabara ya Mlowo - Kamsamba - imekamilika kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 124.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Bw. Hamadi Mbega, aliishukuru Serikali kwa kufanikisha mradi huo, akieleza kuwa utakamilisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Mbozi na Ileje, na kuimarisha usafirishaji wa bidhaa kwenda na kutoka nchi jirani ya Malawi.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Bw. Jabiri Makame, alisema mradi huo utarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji, kufungua fursa za kiuchumi na kuinua maisha ya wananchi. “Tunakushukuru sana Mhe. Rais kwa kutuwezesha kuwapangia kazi makandarasi wazawa, hususan wanawake. Fedha wanazolipwa zitabaki nchini na kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema, huku akiwapongeza wanachama wa Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania kwa kupata mradi huo.

Rais wa Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania, Mhandisi Judith Odunga, aliwahakikishia Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuwa kampuni zao - JUDEX Contractors Ltd na Ibra Contractor Ltd - zitakamilisha kazi kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika, kila moja ikijenga kilomita 5.

Mhandisi Maida Waziri, mmoja wa wakandarasi, alisema watahakikisha wanazingatia kanuni zote za ujenzi, na kwa kiasi kikubwa kuwatumia wanawake wa eneo husika katika shughuli mbalimbali za mradi huo.

Mkuu wa Mkoa aliwataka makandarasi wote kuhakikisha wanatekeleza mradi huo kwa ufanisi, ubora, na kwa muda uliopangwa, huku TANROADS ikisalia kuwa msimamizi wa karibu ili kuhakikisha malengo yanatimia.