UJENZI WA DARAJA LA SANGE ILEJE WAENDELEA KWA KASI
Songwe
12 Agposti, 2025
Ujenzi wa Daraja la Sange wilayani Ileje, mkoani Songwe, unaendelea kwa kasi ambapo kwa sasa mkandarasi yupo katika hatua ya uwekaji wa nguzo 30 za daraja.
Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga, alisema daraja hilo litakuwa na urefu wa mita 25 na litakuwa kiunganishi muhimu kati ya mikoa ya Mbeya na Songwe, na litachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa mikoa hiyo pamoja na Taifa kwa ujumla.
“Daraja hili ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara na bidhaa nyingine kati ya mikoa hii miwili, jambo litakalowezesha ukuaji wa biashara na uchumi, na daraja hili linajengwa kuhimili magari ya tani nyingi,” alisema Mha. Bishanga.
Kwa upande wake, Mha. Noel Mwakapala kutoka kampuni inayoitekeleza mradi huo, alisema daraja litakuwa na urefu wa mita 25 na kazi ya sasa inalenga kuweka nguzo zote 30 kama sehemu ya maandalizi ya juu ya ujenzi.
Daraja la Sange linatarajiwa kupunguza changamoto za usafirishaji hususan nyakati za mvua, ambapo mara nyingi wananchi wamekuwa wakikwama kuvuka kutokana na maji kujaa hususan kipindi cha mvua.