TANROADS KILIMANJARO YAANZA UTEKELEZAJI MIRADI YA DHARURA ILIYOTOKANA NA ATHARI ZA MVUA ZA EL-NINO
Kilimanjaro
10 Agosti, 2025
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kilimanjaro imeanza utekelezaji wa miradi ya dharura kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa za El-Niño mwishoni mwa mwaka 2023, kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 16.
Meneja wa TANROADS mkoani humo, Mhandisi Motta Kyando, amesema miradi hiyo inalenga maeneo manne yaliyoathirika zaidi ambayo ni Kwa Msomali (Msomali), Kileo (Kileo), Kifaru & Saweni (Kifaru & Saweni) na Hedaru (Hedaru), ambapo amesisitiza kuwa serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 16 kufanikisha miradi hiyo.
Katika eneo la Kileo, changamoto kubwa ilikuwa maji kupita juu ya barabara, hali iliyosababisha watumiaji kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kuvuka.
Usanifu uliofanywa na kampuni ya Interconsult ulipendekeza ujenzi wa madaraja ya muundo wa boksi (box culverts bridges) saba yenye ukubwa wa mita 5 kwa 2.5, pamoja na kuinua tuta la barabara kwa mita 1.5 katika kipande chenye urefu wa mita 1,600.
Hadi sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 31, ambapo madaraja matano yamekamilika na mawili yako katika hatua za mwisho za ujenzi, huku kazi ya kunyanyua tuta ikianza katika maeneo yaliyokamilika.
Mradi huo ni sehemu ya mpango wa dharura wa CERC na unatekelezwa na mkandarasi mzawa, King’s Builders, kwa gharama ya shilingi bilioni 5.84. Mkandarasi amepokea malipo ya awali ya shilingi bilioni 2.06, na unatarajiwa kukamilika Septemba 4, 2025.
Kwa upande wa Hedaru, kazi inahusisha kubadilisha daraja dogo la Washi (Mto Washi) na kujenga daraja kubwa la muundo wa boksi (box culvert bridge) lenye midomo miwili, kila mmoja ukiwa na upana wa mita 5 na kimo cha mita 2.5 (2×5×2.5).
Daraja jipya limeshakamilika pamoja na kazi ya kuinua tuta kwa urefu wa mita 675 na kimo cha mita 1.5. Utekelezaji umefikia asilimia 55, na hatua zilizosalia ni kuweka tabaka la msingi (CRR), tabaka la lami na kumalizia alama za barabarani pamoja na michoro (road markings).
Mradi huu unatekelezwa na mkandarasi mzawa, JP Traders, kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5, ambapo malipo ya awali yaliyotolewa ni shilingi 224,255,782.80.