News

TANROADS YAWEZESHA MAFUNZO KWA WATUMISHI WA MZANI KATIKA DARAJA LA KIGAMBONI

TANROADS YAWEZESHA MAFUNZO KWA WATUMISHI WA MZANI KATIKA DARAJA LA KIGAMBONI

Dar es Salaam

09 Agosti, 2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendesha mafunzo maalum kwa watumishi wa kituo cha mzani cha Daraja la Mwalimu Julius Nyerere, Kigamboni, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhandisi Vicent Tarmo kutoka Kitengo kinachosimamia shughuli za mizani TANROADS Makao Makuu, amesema mafunzo yamehusisha Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.

Amebainisha kuwa washiriki ni wafanyakazi ambao awali walikuwa chini ya usimamizi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) lakini sasa watakuwa rasmi chini ya TANROADS kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo na miongozo yake.

 

“Tumeweza kuwapa elimu ya udhibiti uzito, taratibu za mizigo mipana na mizigo maalum, pamoja na vibali vinavyotolewa na Wizara ya Ujenzi kupitia Kitengo cha Usalama na Mazingira. Pia tumewafundisha maadili ya utumishi wa umma na kuwapa nafasi ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi,” alisema Mha. Tarmo.

Aidha, washiriki wametembelea kituo cha mzani cha Kigamboni kuona namna kazi inavyotekelezwa na kupewa maelekezo ya kusimamia majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Mafunzo hayo, yaliyofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9 Agosti, 2025, yamewezeshwa na wakufunzi kutoka Wizara ya Ujenzi, TANROADS Makao Makuu, na Ofisi ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kwa upande wake, Afisa kutoka Wizara ya Ujenzi, Mha. Mrisho Kamakole, amesema ametoa mafunzo kuhusu namna ya kupata vibali vya mizigo maalum kupitia tovuti ya Wizara, akisisitiza kuwa wasafirishaji lazima wakidhi matakwa ya sheria kabla ya kusafirisha mizigo ya aina hiyo.

Ameongeza kuwa washiriki wameelewa vyema masuala hayo na anatarajia kuyaweka katika vitendo ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria unafanyika ipasavyo.