News

TANROADS YAWAKUMBUSHA WATUMISHI WAPYA WA MIZANI KUZINGATIA MAADILI KAZINI

TANROADS YAWAKUMBUSHA WATUMISHI WAPYA WA MIZANI KUZINGATIA MAADILI KAZINI 

Dar es Salaam

08 Agosti, 2025

Afisa Rasilimali Watu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Makao Makuu, Edgar Edward Msigala, ametoa wito kwa watumishi wa mizani kuhakikisha wanazingatia maadili, nidhamu na kanuni za kazi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa mizani katika Daraja la Mwalimu Nyerere, Kigamboni, Msigala amesema maadili ni msingi wa maisha na kazi, na kuyazingatia huboresha utendaji na kuongeza heshima ya taasisi mbele ya jamii. 

“Unapomkumbusha mtumishi katika maadili, unamkumbusha mwenendo, sheria, taratibu, kanuni na miongozo. Akizingatia haya yote, utulivu na utendaji wake hubadilika; atakuwa mwadilifu, mtiifu, anazingatia muda na kufuata taratibu za kazi,” alisema Msigala. 

Ameongeza kuwa nidhamu na maadili mazuri hujenga taswira chanya kwa wananchi, hasa kwa watumishi wa mizani ambao huduma zao huonekana moja kwa moja na jamii.

Amesema, huduma bora kwa wateja huimarisha imani ya wananchi na kujenga picha nzuri ya serikali. 

Msigala pia amebainisha kuwa, serikali imeweka mifumo ya kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi, ikiwemo mfumo wa E-Mrejesho unaomwezesha mteja kutoa maoni, pongezi au malalamiko moja kwa moja kwa mwajiri, hatua inayosaidia kuboresha huduma. 

Akiwakumbusha watumishi wote wa umma, amesema ni muhimu kila mmoja kujitathmini binafsi kuhusu mwenendo wake bila kusubiri uangalizi wa mtu mwingine. 

“Ni lazima tujiulize, je, nipo sehemu sahihi? Je, ninachofanya kinalingana na miongozo ya mwajiri wangu? Utendaji bora huanza na kujiongoza binafsi,” alisisitiza.

 Kwa mujibu wa Msigala, mafunzo hayo yamelenga kuongeza uelewa wa watumishi kuhusu maadili na nidhamu, ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora na kwa viwango vinavyotarajiwa.