USAFIRISHAJI SALAMA WA KEMIKALI WAPEWA KIPAUMBELE KATIKA MAFUNZO YA WATENDAJI WA MIZANI
Dar es Salaam
07 Agosti, 2025
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeandaa mafunzo maalum kwa watendaji wa mzani katika daraja la Mwalimu Julius Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu usafirishaji salama wa kemikali.
Katika mafunzo hayo, Stephano Nguvagulu, Mkaguzi wa Kemikali kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, amewasilisha mada kuhusu usafirishaji wa kemikali, akieleza kuwa shughuli hiyo inasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Majumbani na Viwandani Na. 3 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake za mwaka 2015 na zilizoboreshwa mwaka 2020.
Nguvagulu amegusia masuala mbalimbali muhimu ikiwemo vigezo vya kisheria kwa wasafirishaji wa kemikali, sifa za magari yanayopaswa kusafirisha kemikali, pamoja na mbinu bora za upakiaji, upakuaji na upimaji wa mizigo ya kemikali, hasa inapofika kwenye mizani.
Pia ametoa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na umwagikaji wa kemikali, na kufafanua aina ya tozo na faini zinazotolewa kwa mujibu wa sheria kwa kampuni au mtu binafsi atakayekiuka taratibu. Alisema kuwa kuacha kemikali barabarani kunagharimu faini ya Shilingi milioni 15.
“Shughuli za kemikali zimeongezeka sana nchini kutokana na ongezeko la mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam, inayosafirishwa kwenda nchi jirani kama Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Malawi. Ni muhimu kuwa na uelewa wa pamoja kati ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na watendaji wa mizani katika kuhakikisha usafirishaji unafanyika kwa usalama,” alieleza Nguvagulu.
Kwa upande wake, Afisa Mizani wa Daraja la Julius Nyerere, Rahma Shabani, ameishukuru TANROADS kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yamewajengea uwezo mkubwa wa kitaalamu na kuwapa mwanga mpya katika utendaji wao wa kila siku.
“Mafunzo haya yametupa elimu kubwa na mwongozo wa kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Tunaamini baada ya mafunzo haya, utendaji kazi utakuwa bora kuliko awali. Tunaomba TANROADS iendelee kutupatia mafunzo haya mara kwa mara,” alisema Rahma.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za TANROADS katika kuimarisha usalama wa usafirishaji wa kemikali nchini, kwa kushirikiana na taasisi husika na wadau wa usalama barabarani.