MAFUNZO YA TANROADS YAONGEZA UWEZO WA WAFANYAKAZI WA MZANI KATIKA DARAJA LA MWALIMU NYERERE
Dar es Salaam
06 Aug, 2025
Wafanyakazi wa mzani katika Daraja la Mwalimu Julius Nyerere lililopo Kigamboni, jijini Dar es Salaam, wameeleza kufaidika na mafunzo maalum waliyopatiwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), yakilenga kuongeza ufanisi na uelewa kuhusu sheria na usimamizi wa miundombinu ya barabara.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, wafanyakazi hao wamesema kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kupata mwelekeo mpya wa kikazi na kuwaandaa kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi.
"Kwa ujumla tuna utofauti mkubwa sana katika mafunzo tunayopata, tumeongeza maarifa na ujuzi wa hali ya juu. Tunawashukuru TANROADS kwa kutupatia mafunzo. Tukitoka hapa tutakuwa na mwelekeo mpya zaidi," alisema Awetu Salim Amri, mmoja wa wafanyakazi wa mzani katika daraja hilo.
Naye Tulapewa Abel Mheni, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesema kuwa:
"Tunatarajia mafunzo tuliyoyapata yatatusaidia kuboresha utendaji kazi wetu katika kituo chetu cha kazi cha mzani."
Kwa upande wake, Afisa Mizani, Hussein Mchowera, ameeleza kuwa mafunzo hayo yameongeza ufanisi kwa watumishi na kuongeza ari ya kuwahudumia wananchi kwa uadilifu:
"Nitoe shukrani kwa viongozi wetu kwa kutuandalia mafunzo haya ambayo kwa namna moja yametuongezea ufanisi katika utendaji wetu wa kazi."
Julius Rweyongeza, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa ajili ya kulinda miundombinu na kutekeleza sheria kwa ufanisi:
"Natoa shukrani za dhati kwa TANROADS ambao wametupa mafunzo juu ya sheria za barabara. Tunatarajia kuyafanyia kazi ili kulinda miundombinu inayosimamiwa na TANROADS, mfano pale katika daraja la Mwalimu Nyerere."
"Tutahakikisha tunasimamia vyema majukumu yetu kwa mujibu wa mafunzo tuliyopata pamoja na kutekeleza sheria zote. Naomba tuendelee kupewa mafunzo ya kukumbushana mara kwa mara ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi," aliongeza.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa TANROADS wa kuimarisha uwezo wa wafanyakazi wake katika vituo vya mizani ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa miundombinu ya barabara nchini.