WATENDAJI WA MIZANI KATIKA DARAJA LA MWALIMU JULIUS NYERERE WAPEWA MAFUNZO YA SHERIA NA TARATIBU ZA UDHIBITI UZITO WA MAGARI
Dar es Salaam
05 Aug, 2025
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Kitengo cha Mizani Makao Makuu, imeanza kutoa rasmi mafunzo ya siku tano kwa watendaji wa mizani katika daraja la Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yanafuatia uamuzi wa Serikali kuhamishia rasmi usimamizi wa mzani huo kutoka taasisi nyingine na kuupeleka chini ya usimamizi wa TANROADS.
Mafunzo hayo yameanza leo tarehe 5 Agosti na yanatarajiwa kukamilika tarehe 9 Agosti 2025, yakilenga kuwawezesha watendaji waliopo kufahamu na kuendana na mifumo ya kiutendaji, sheria, kanuni na miongozo ya TANROADS kama taasisi yenye dhamana ya usimamizi wa mizani yote nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo hayo, Mhandisi Vicent Tarmo kutoka Kitengo cha Mizani – TANROADS Makao Makuu amesema:
“Mafunzo haya yamelenga kuwawezesha watendaji waliopo katika mzani huu kuendana na miongozo ya TANROADS kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake za mwaka 2018. Tunawapa nyenzo za kiutendaji zitakazowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria.”
Ameongeza kuwa, mafunzo hayo yanahusisha pia taratibu za usimamizi wa mizigo maalumu, miongozo ya kiutendaji inayotumika ndani ya TANROADS, pamoja na mafunzo kwa vitendo katika mzani huo uliopo Kigamboni kwa lengo la kuwapa uzoefu wa moja kwa moja.
Kwa upande wake, Mhandisi Leonard Saukwa kutoka Wizara ya Ujenzi amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kuhakikisha kuwa mizani zote muhimu nchini zinasimamiwa na taasisi moja yenye uwezo wa kitaalamu, na hivyo kupeleka mzani wa daraja la Mwalimu Nyerere chini ya TANROADS.
“Lengo la Serikali ni kulinda barabara zetu dhidi ya uharibifu unaotokana na magari yanayozidisha uzito. Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo ilianza kutumika nchini kuanzia Machi 1, 2019, ndiyo msingi wetu. Hivyo, tunawapa mafunzo watendaji hawa ili waendane na mfumo wa usimamizi mpya,” alisema Mhandisi Saukwa.
Naye Afisa Sheria kutoka TANROADS Makao Makuu, Baraka Maugo, amebainisha kuwa sheria hiyo mama ya Afrika Mashariki imeeleza kwa kina vipengele vyote vinavyohusu uzani wa magari, makosa yanayoweza kufanywa na wadau wa usafirishaji, na wajibu wa maafisa wa mizani.
“Tunasisitiza pia umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu sheria hizi ili kuhakikisha usimamizi wa uzito barabarani unafanyika kwa usawa na haki. Mafunzo haya ni msingi wa kujenga maafisa wenye uelewa wa kisheria, kiutendaji na kimaadili,” alisema Maugo.
Kwa pamoja, viongozi hao wameeleza kuwa hatua ya kupeleka mzani huo chini ya TANROADS inalenga kuongeza ufanisi, uwajibikaji, na ulinzi wa miundombinu ya barabara kwa kutumia mifumo ya kisasa na wataalamu waliopata mafunzo maalumu.
Kupitia hatua hii, TANROADS inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuimarisha mifumo ya usimamizi wa barabara kwa kutumia wataalamu wenye weledi, huku ikizingatia sheria, miongozo na uwajibikaji. Mafunzo haya si tu yanaboresha utendaji wa kila siku wa maafisa wa mizani, bali pia yanaimarisha ulinzi wa barabara kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi kwa taifa zima.