KAHAMA-KAKOLA YAFUNGUKA KWA LAMI CHINI YA USIMAMIZI MADHUBUTI WA TANROADS.
Shinyanga
02/08/2025
Shinyanga inaendelea kuimarika kimkakati kupitia maendeleo ya miundombinu, huku Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ukiongoza kwa umahiri usimamizi wa ujenzi wa barabara ya Kahama–Kakola yenye urefu wa kilometa 73 kwa kiwango cha lami.
Ujenzi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi, kuhakikisha barabara za kimkakati zinajengwa kwa ubora na kwa wakati, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika sekta za madini, kilimo na biashara kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kwa mujibu wa Mhandisi Marco Bee kutoka Kitengo cha Ushauri wa Uhandisi cha TANROADS (TECU), mradi huu unaendelea kutekelezwa kwa kasi chini ya usimamizi wa karibu wa TANROADS, ambapo hadi sasa umefikia asilimia 32.94 ya utekelezaji.
“TANROADS tunasimamia kwa ukaribu kila hatua ya ujenzi ili kuhakikisha mkandarasi anakamilisha kazi kwa ubora unaotakiwa na ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba,” alieleza Mhandisi Bee.
Mradi unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick Gold Mine kwa gharama ya shilingi bilioni 100.6, huku kazi ikifanywa na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa muda wa miezi 27.
TANROADS kupitia timu yake ya wataalamu wa TECU imehakikisha kuwa hatua zote za kiufundi zinafuatwa, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa matabaka ya msingi (tuta), makalavati, na tabaka la saruji. Katika hatua zijazo, mradi utajumuisha pia ujenzi wa vituo vya daladala na uwekaji wa taa za barabarani ili kuimarisha usalama na huduma kwa watumiaji.
“Mradi huu ukikamilika utafungua fursa kubwa za kiuchumi, hasa katika sekta ya madini na kilimo kwa mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu na Kagera,” alisema Mhandisi Bee.
Aidha, TANROADS imesisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii, ambapo zaidi ya Watanzania 387 wamepata ajira kupitia mradi huu—ikiwa ni moja ya mafanikio ya kiuchumi ya moja kwa moja yanayoletwa na miradi ya miundombinu inayosimamiwa na Wakala huo.
Akihitimisha, Mhandisi Bee aliipongeza Serikali na Wizara ya Ujenzi kwa kuweka mazingira bora ya utekelezaji na kuahidi kuwa TANROADS itaendelea kusimamia mradi huu kwa umakini mkubwa hadi utakapo kamilika kwa ubora wa hali ya juu.
“TANROADS tumejipanga kikamilifu kuhakikisha kazi hii inakamilika kwa wakati, kwa viwango vilivyokubaliwa, na kwa manufaa ya Watanzania wote,” alisisitiza.