News

TANROADS KWA USHIRIKIANO NA NIT YAENDESHA MAFUNZO YA USALAMA BARABARANI KWA WAHANDISI

TANROADS KWA USHIRIKIANO NA NIT YAENDESHA MAFUNZO YA USALAMA BARABARANI KWA WAHANDISI

Dar es salaam

26/07/2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), wameendesha mafunzo kitaalamu ya Ukaguzi wa Usalama Barabarani (Road Safety Audit) kwa wahandisi wa TANROADS kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Mafunzo hayo ya siku kumi yamefadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Barabara (International Road Federation – IRF) kutoka Uswisi kwa kushirikiana na Total Energies Foundation, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kuboresha viwango vya usalama katika miundombinu ya barabara.

Kozi hiyo ya kitaalamu ilihusisha washiriki 23 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Arusha, Mwanza, Songwe na Kagera.

Lengo kuu la mafunzo hayo lilikuwa kuwajengea uwezo wataalamu hao kuainisha mapungufu ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, viashiria vya hatari na ajali zinazoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara, pamoja na kuandaa mapendekezo ya kiufundi ya kuzuia ajali na kupunguza madhara kwa jamii.

Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa mtindo wa nadharia na vitendo chini ya usimamizi wa wakufunzi waliobobea kutoka IRF wakiongozwa na Mhandisi Miguel  Santos na Laurent Maganga.

Washiriki wa mafunzo hayo, walipata ujuzi wa kisasa wa kufanya tathmini za usalama barabarani na walitunukiwa vyeti vya kitaifa na kimataifa vinavyotambulika katika nyanja ya ukaguzi wa usalama wa miundombinu ya Barabara duniani.

Kwa mujibu wa TANROADS, hatua hii ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha uwezo wa wataalamu wake wa ndani ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi.

Aidha, inatarajiwa kuwa mafunzo hayo yataongeza thamani ya rasilimali watu ndani ya taasisi kwa kuendana na mabadiliko ya kitaalamu na kiteknolojia katika sekta ya miundombinu hususani kwenye Usalama wa barabara ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.

Kupitia ushirikiano wa kimataifa kama huu, TANROADS inaendelea kuimarisha mazingira ya kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora na usalama.

Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya muda mrefu ya kuboresha sekta ya barabara nchini kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.